SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Alhamisi, 12 Aprili 2018

T media news

Spika Ndugai Aitupilia Mbali Hoja ya Kubenea

Spika wa Bunge, Job Ndugai ameitupilia mbali hoja ya Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea (Chadema) kuhusiana na marekebisho ya masuala yanayohusu Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Akizungumza bungeni mjini Dodoma leo Alhamisi Aprili 12, Spika Ndugai amesema Kubenea alileta kusudio la kuwasilisha hoja binafsi bungeni akitaka bunge lifanye marekebisho ya masuala yanayohusiana na NEC.

“Ili ikidhi matakwa ya mfumo wa vyama vingi hapa nchini sasa kwa kuwa Tume hiyo ya Taifa ya Uchaguzi imeanzishwa na Katiba katika Ibara ya 74 marekebisho yote juu ya tume hiyo yanatakiwa kuletwa kwa kupitia muswada wa marekebisho ya Katiba na si hoja binafsi ya Mbunge.

“Nafikiri naeleweka katika ninachokisema unapoleta jambo ambalo linahusu Katiba basi upo utaratibu wa kufuata ili iendane na marekebisho ya katiba na siyo hoja tu ya Mbunge.

“Kwa hiyo kwa kuwa kanuni ya 58 kanuni ndogo ya kwanza ya Bunge imenipa madaraka ya kukataa hoja inayovunjwa Katiba.

“kwa hiyo taarifa yako Mheshimiwa Kubenea naikataa kwa hiyo kajipange tena, kama bado una nia, uje katika utaratibu unaotakiwa kama hatukukuelewa tutatafuta muda ili tueleweshane zaidi ila sisi tumeelewa hivyo,” amesema Spika Ndugai.