SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumapili, 4 Machi 2018

T media news

Simba Msiandae Nyimbo za Ubingwa, Safari Bado Ndefu

Na Baraka Mbolembole

Kwa  mara nyingine Simba SC imepata ‘sare ya kufadhaisha na kukatisha’ tamaa, lakini matokeo ya 3-3 katika uwanja wa Taifa, Dar es Salaam dhidi ya Stand United yanaendelea kudhihirisha maneno yangu kuwa mabingwa hao wazamani ‘hawana’ kikosi chenye ubora, mbinu na uwezo wa kurudisha taji la ligi kuu ambalo wanasotea kwa msimu wa sita sasa.

Bila Okwi, Bocco

Baada ya mchezo wa raundi ya 18 dhidi ya Mwadui FC 2-2 Simba niliandika makala kuelezea namna timu hiyo ilivyo dhaifu katika mashambulizi hasa pale alipoumia nahodha John Bocco. Kukosekana kwa pamoja wafungaji wao namba moja, (Emmanuel Okwi na Bocco) katika mchezo wa jana dhidi ya Stand kuliwafanya wageni hao kutocheza kwa hofu yoyote.

Kabla ya kuanza kwa mchezo nilimsikia kocha msaidizi wa Simba, Mrundi, Masoud Djuma akisema kuwa wamehofia kuwatumia washambuliaji hao wawili kutokana na uwepo wa mchezo wa Confederation Cup dhidi ya Wamisri, Al Masry siku ya Jumatano ijayo. Okwi aliumia katika mchezo wa raundi ya 19 Simba 5-0 Mbao FC, wakati Bocco bado hajarejea kikosini tangu alipopata majeraha ya enka katika mchezo vs Mwadui.

Kukosekana kwao kulitoa nafasi ya Mrundi, Laudit Mavugo kurejea katika kikosi cha kwanza na licha ya kwamba alifanikiwa kufunga goli lake la tatu msimu huu, alishindwa kutengeneza muunganiko  mzuri na Nicholas Gyan baadae akatolewa baada ya kupata majeraha na nafasi yake kuchukuliwa na mshambulizi mwingine asiye na makali, Juma Ndanda Liuzio.

Katika andiko langu lililopita, ‘Simba hawatacheza nyimbo za ubingwa msimu huu’ Nilielezea wasiwasi wangu kuhusu kikosi hicho cha Mfaransa, Pierre Lechantre hasa pale kitakapolazimika kucheza bila huduma ya Bocco na Okwi. Katika michezo ya karibuni timu pinzani zimekuwa zikiwahofia sana wafungaji hao waliofunga jumla ya magoli 26 katika VPL, na kutokuwepo kwao kunawafanya wapinzani kujiamini zaidi, huku Simba wakikosa makali.

Bance atawaumiza kwa beki hii ya Mlipili & Nyoni

Shomari Kapombe alihusika katika moja ya magoli ya Stand United kutokana na umakini wake mdogo, golikipa Aishi Manula ameendelea kuonyesha kiwango cha chini baada ya kuruhusu goli la kona ya moja kwa moja lakini matatizo yote katika ngome ya timu hiyo yanasabishwa na safu ya beki ya kati kushindwa kucheza  kwa maelewano mazuri.

Yusuph Mlipili na Erasto Nyoni si wachezaji ambao wanaweza kukupa matokeo mazuri wanapocheza pamoja kwa sababu naamini walinzi hao wa kati wote wanahitaji mtu ambaye ametulia zaidi na kuwaongoza. Wawili hawa wote wanapenda kukaba na jambo hili linaweza kuwahukumu vibaya vs mshambulizi wa Al Masry, Bance siku ya Jumatano.

Waliporuhusu magoli mawili dhidi ya Mwadui FC niliandika namna safu ya ulinzi ya Simba ilivyo dhaifu hasa pale inaposhambuliwa. Stand wamedhihirisha hilo na bila njia mbadala Simba wasitaraji kupata chochote msimu huu. Kuruhusu magoli matano katika michezo mitatu iliyopita huku magoli matatu yakifungwa uwanja wa Taifa ni ‘ujumbe’ sahihi kwa benchi la ufundi la timu hiyo kuhusu ngome yao ambayo wamekuwa wakijinasibu ni bora kuliko msimu huu.

Kama hawatabadili mbinu zao za kujilinda sina shaka yoyote kuwa Waarabu toka Misri watafunga si chini ya magoli matatu katika uwanja wa Taifa siku ya Jumatano ijayo, lazima Simba waanze kuandaa mbinu zao za kujilinda. Wiki iliyopita niliandika pia ili ufanikiwe kuwa bingwa wa ‘ligi’ kuna wakati huitaji kucheza vizuri zaidi ya kupata alama tatu tu, na unapaswa kuwa mjinga na kukubali kucheza mchezo wa kujilinda ili kulinda uongozi wao wa mchezo.

Nini malengo yao?

Kwa taarifa nilizozipata ni kwamba Okwi na Bocco wote walikuwa na uwezo wa kucheza vs Stand United lakini benchi la ufundi liliwachukilia wapinzani wao kama timu isiyoweza kuwasumbua kwa lolote ndiyo maana wakaamua kuwatumia washambuliaji ambao ‘hawakuwa tayari.’ Je, Simba wamebadili malengo yao msimu huu?

Inaonekana akili yao wameipeleka Caf jambo ambalo hawakupaswa kulifanya kwa maana malengo ya msimu huu ni kurudisha ubingwa wa VPL si vinginevyo. Kubadili malengo ‘juu kwa juu’ hasa wakati huu wakiwa wanafukuzwa kwa kasi na mabingwa watetezi Yanga SC kunawapoteza kirahisi mno na ni wazi watakuwa katika ‘umbo’ baya baada ya mchezo wa Jumatano ijayo dhidi ya Al Masry.

Simba wanapaswa kutumia nguvu zao zote katika VPL na si kuifadhi nyingine kwa sababu ya michuano ya Caf kwa maana michuano hiyo ni ‘,mikubwa mmno’ kwao msimu huu  hivyo wanaweza kujikuta wakipoteza kila kitu. Wakakosa VPL na kuanguka Caf. Narudia tena, msiandae nyimbo za ubingwa, safari bado ndefu na mashaka ni makubwa.