SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumamosi, 3 Machi 2018

T media news

Mawakili Waiomba Mahakama Iyafute Mashitaka ya Kutakatisha Fedha yanayowakabili Kitilya na Wenzake

MAWAKILI wa utetezi katika kesi inayomkabili Kamishna Mkuu wa zamani wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Harry Kitilya na wenzake wawili wameiomba mahakama kuuamuru upande wa Jamhuri kufuta mashtaka ya utakatishaji fedha ili washtakiwa hao waweze kupata dhamana.

Mbali na Kitilya washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Shose Sinare na ofisa wa benki ya Stanbic, Sioi Solomon.

Madai hayo yalitolewa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Victoria Nongwa, aliyepangiwa kusikiliza kesi hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam.

Upande wa Jamhuri uliongozwa na wakili wa serikali mwandamizi, Mutalemwa Kishenyi.

Upande wa utetezi uliongozwa na mawakili Majura Magafu na Alex Mgongolwa.

Awali, Kishenyi alidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika na kuiomba mahakama kupanga tarehe nyingine ya kutajwa.

Hata hivyo, upande wa utetezi uliomba mahakama kuuamuru upande wa Jamhuri kuwaondolea washtakiwa mashtaka ya kutakatisha fedha kwa sababu wanateseka mahabusu.

Pia, upande huo uliomba kuwa washtakiwa wakifutiwa mashtaka hayo watakua na haki ya kupata dhamana."Mheshimiwa hakimu ni rai yetu upande wa utetezi kwamba kwa kuwa upande wa Jamhuri bado wanadai hawajakamilisha upelelezi, tunaomba leo mahakama yako itoe ahirisho la mwisho," alidai Wakili Magafu.

"Pia mahakama yako iwaamuru wayaondoe mashtaka ya utakatishaji wa fedha ili washtakiwa waweze kupata dhamana kwa kuwa wamekaa mahabusu kwa muda mrefu."

Akijibu hoja za utetezi, wakili Kishenyi alidai kuwa mashtaka yanayowakabili kina Kitilya hayana ukomo wa upelelezi na kwamba bado wanafanya juhudi za kuharakisha ili kesi iendelee.

Hakimu Nongwa alisema upande wa Jamhuri uongeze juhudi za upelelezi kwa kuwa washtakiwa wako mahabusu muda mrefu ili kila upande upate haki yake.

Alisema kesi hiyo itatajwa tena Machi 16 na washtakiwa hao wataendelea kukaa mahabusu.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka ya kula njama, kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha fedha.

Ilidaiwa makosa hayo yalifanyika kati ya Machi 2013 na Septemba 2015 wakati wa mchakato wa mkopo wa dola za Marekani milioni 550 kwa Serikali kutoka Benki ya Standard nchini Uingereza.

Upande wa Jamhuri ulidai kuwa Machi 2013 jijini Dar es Salaam washtakiwa walijipatia dola za Marekani milioni sita wakionyesha kuwa fedha hizo zilikuwa ni malipo ya ada ya uwezeshaji upatikanaji wa mkopo na zililipwa kupitia Kampuni ya Egma T Ltd.

Washtakiwa hao wanadaiwa kutakatisha fedha kwa kuhamisha, kuchukua na kuweka kiasi cha dola za Marekani milion sita katika akaunti tofauti tofauti za benki.

Kati ya Machi 2013 na Septemba 2015, wanadaiwa kuwa waliweka pesa hizo katika akaunti mbalimbali zilizomilikiwa na kampuni ya Egma na kwamba walipaswa kufahamu kuwa pesa hizo ni mazao ya uhalifu wa kughushi.

Machi 12, mwaka jana Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu iliambiwa upelelezi wa kesi unaendelea nje ya nchi ili kukamilisha na kesi iweze kuendelea.

Wakili wa Serikali Esterzia Martin alidai kuwa hatua ya kesi hiyo umebaki upelelezi wa nje ya nchi na kwamba upande wa Jamhuri unaomba tarehe nyingine ya kutajwa.

Washitakiwa hao walipandishwa kizimbani mahakamani hapo kwa mara ya kwanza Aprili mosi, mwaka 2016.