Mbunge wa Singida Mashariki kwa tiketi ya (CHADEMA) Mhe. Tundu Antiphas Lissu amefunguka na kusema amefarijika sana kutembelewa na Mbunge wa Tandahimba (CUF) Katani Ahmad Katani na kudai mbunge huyo alikuwa miongoni mwa watu waliompeleka Nairobi.
Lissu ameeleza hayo kupitia ukurasa wake maalumu wa kijamii na kusema mbali na kumlijua hali lakini waliweza kujadiliana kuhusu mwenendo wa siasa zinazoendelea nchi Tanzania.
"Mheshimiwa Katani amekuja Ubelgiji kunijulia hali pamoja na kuja kujadiliana nami masuala mbali mbali yanayohusu siasa za nchi yetu na mustakbali wa Taifa letu. Katani alikuwa kwenye msafara wa Wabunge walionipeleka Nairobi, Kenya, mara baada ya jaribio la mauaji la September 7, na alikaa Nairobi kwa siku nne. Nimefarijika sana na ugeni huu wa ndugu yangu na kaka yangu Katani", amesema Lissu.
Mbunge Tundu Lissu alishambuliwa na watu wasiojulikana tangu Septemba 7,2017 akiwa mkoani Dodoma, na kisha kupelekwa nchini Nairobi kwa matibabu na baada ya miezi 3 alipelekwa nchini Ubelgiji kwa hatua nyingine ya matibabu.