Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametoa wito kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kusimamia vizuri rasilimali walizonazo na kukusanya kodi vizuri ili waweze kutekeleza miradi mikubwa ya ujenzi wa miundombinu na kuimarisha huduma za afya kwa wananchi.
Mhe. Rais Magufuli ametoa wito huo leo tarehe 22 Februari, 2018 mjini Kampala nchini Uganda wakati akichangia katika mkutano wa wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki unaojadili maendeleo na upatikanaji wa fedha kwa ajili ya miradi ya sekta ya miundombinu na afya.
Kabla ya Mhe. Rais Magufuli kutoa mchango wake, Marais walioshiriki mkutano huo wamepokea taarifa ya mkutano wa majadiliano ya kisekta (Round Table) kuhusu mahitaji ya fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya sekta ya miundombinu na afya ambapo imeelezwa kuwa katika miaka 10 ijayo nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zitahitaji Dola za Marekani Bilioni 78 kutekeleza miradi ya miundombinu inayopendekezwa.
Taarifa hiyo imechangiwa na wadau mbalimbali wakiwemo Marais, wawakilishi wa sekta binafsi na washirika wa maendeleo ambao wameelezea njia mbalimbali za kupata fedha za kutekeleza miradi hiyo ikiwemo kutumia mfumo wa ushirikiano kati ya Serikali na Sekta binafsi (PPP).
Katika mchango wake Mhe. Rais Magufuli amesema pamoja na kutumia mfumo wa PPP ni muhimu kwa Serikali za kila nchi kusimamia vizuri ukusanyaji wa mapato ya kodi na rasilimali nyingine ili kutekeleza miradi ya miundombinu, afya na sekta nyingine.
Ametahadharisha kuwa japo kuwa mfumo wa PPP ni mzuri, ni vyema wataalamu wakachukua tahadhali za kutosha ili kuepusha Serikali kuingia katika mikataba isiyokuwa na maslahi kwa nchi zao kutokana na baadhi ya wadau wa sekta binafsi kutaka kutengeneza faida kubwa kwa kupandisha gharama za miradi.
Mhe. Rais Magufuli ametolea mfano wa miradi mikubwa iliyoanza kutekelezwa nchini Tanzania ukiwemo ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (Standard Gauge) na ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme katika maporomoko ya mto Rufiji (Stieglers’ Gorge), kuwa Serikali ya Tanzania imeamua kuanza kutekeleza miradi hiyo kwa kutumia fedha zake baada ya kufanikiwa kusimamia vizuri rasilimali zake na kubana matumizi.
“Mimi naamini tukiamua tunaweza, nchi zetu zina rasilimali nyingi za kuweza kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, mathalani tafiti zinaonesha kuwa kama nchi zetu zitaweza kukusanya vizuri mapato ya kodi, zinaweza kutekeleza nusu ya miradi yake ya maendeleo.
“Lakini ukiachilia mbali mapato ya kodi, tunapoteza fedha nyingi kupitia utoroshaji wa rasilimali zetu, ripoti ya jopo la Umoja wa Afrika lililoongozwa na Rais Mstaafu wa Afrika Kusini Mhe. Thabo Mbeki imeeleza kuwa nchi za Afrika zinapoteza Dola za Marekani Bilioni 150 kila mwaka kutokana na utoroshaji wa rasilimali” amesema Mhe. Rais Magufuli.
Marais waliohudhuria mkutano huo ni Rais wa Uganda Mhe. Yoweri Kaguta Museveni, Rais wa Kenya Mhe. Uhuru Muigai Kenyatta, Rais wa Sudan Kusini Mhe. Salva Kiir Mayardit na Marais wa Rwanda na Burundi wamewakilishwa.
Kesho tarehe 23 Februari, 2018 Mhe. Rais Magufuli atahudhuria mkutano wa 19 wa wakuu wa nchi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Kampala
22 Februari, 2018