SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Alhamisi, 22 Februari 2018

T media news

Serikali yatangaza hatma ya watumishi walioachwa katika orodha ya wanaostahili kulipwa madeni yao

Serikali imewaondoa hofu watumishi ambao hawakuwamo katika orodha ya kwanza ya malipo ya madeni kwa kusema uhakiki wa malipo zaidi unaendelea na majina mengine yataendelea kutangazwa.

Aidha, serikali imewataka watumishi wenye madai lakini hawajawasilisha nyaraka zake kuzipeleka kwa waajiri wao haraka ili waingizwe katika orodha nyingine za malipo.

Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dkt Laurean Ndumbaro alitoa ufafauzi huo kutokana na kuwepo kwa sitfahamu ya hatima ya watumishi wa umma ambao hawakuwamo katika orodha ya malipo iliyotoka.

Febaruari 9, serikali ilitangaza kulipa madai ya watumishi wa umma ya Sh. bilioni 43.39 pamoja na mshahara mwezi huu.

Akitangaza malipo hayo mjini Dodoma, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt Philip Mpango alisema baada ya kufanya uhakiki wa kina wa madeni hayo, serikali ilibaini kuwa watumishi 27,389 kati ya 82,111 ndiyo wanastahili kulipwa jumla ya Sh 43,393,976,807.23.

Ilielezwa kuwa malipo hayo ni asilimia 34 ya madai yote ya zaidi ya Sh. bilioni 127.61 yaliyohakikiwa na kuonekana ni sahihi na yanastahili kulipwa bila marekebisho.

Dkt Ndumbaro alieleza kuwa, serikali inaendelea na uhakiki wa madai na pindi yatakapokamilika yatalipwa yote.

“Orodha bado zinaendelea kwa sababu uhakiki bado unaendelea, ni zoezi endelevu. Hatuwezi kufahamu list (orodha) ngapi zitatolewa kwa sababu waajiri bado wanaendelea na uhakiki wa madai,” alisema Dkt Ndumbaro.

Alisema orodha ya watumishi wanaoidai serikali iliyotoka ni ile iliyowahusu watumishi waliohakikiwa na kubainika hawana matatizo yoyote.

Alisema uhakiki wa orodha hiyo ni mkubwa kwa sababu umehusu watumishi wengi kutoka katika idara nyingi.

Alieleza kuwa kuna watumishi wa umma wengine wameshahakikiwa madeni yao lakini fomu zao zilibainika kuwa na matatizo, hivyo waajiri wao wanazirekebisha.

“Watumishi wengine wanaendelea kuzileta, kwa hiyo uhakiki bado unaendelea na madai yataendelea kulipwa. Ni zoezi endelevu,” alisema.

Akizungumza siku hiyo mjini Dodoma, Dkt Mpango alisema serikali kupitia mfumo wa taarifa za kiutumishi na mishahara ilibaini kufikia Julai 1, 2017 ilikuwa na madai ya malimbikizo ya mishahara yenye jumla ya Sh. 127,605,128,872.81 kwa watumishi 82,111.

Dkt Mpango alisema kati ya watumishi hao, walimu walikuwa 53,925 waliokuwa wanadai Sh. 53,940,514,677.23 sawa na asilimia 42.27 ya madai yote na wasiokuwa walimu walikuwa 28,186 waliokuwa wanadai Sh. 73,664,614,195.58 sawa na asilimia 57.73.

“Madai haya yalijumuisha mishahara isiyolipwa, tofauti ya mishahara kutokana na kukaimu na nyongeza za mishahara zilizotokana na kupandishwa vyeo na kuchelewa kurekebishiwa mishahara,” alisema Dkt Mpango.