SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Ijumaa, 23 Februari 2018

T media news

Rais Magufuli atoa wito Jumuiya ya Afrika Mashariki

Rais Dkt. John Pombe Magufuli ametoa wito kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kusimamia vizuri rasilimali walizonazo na kukusanya kodi vizuri ili waweze kutekeleza miradi mikubwa ya ujenzi wa miundombinu na kuimarisha huduma za afya kwa wananchi.

Rais Magufuli ametoa wito huo mjini Kampala Uganda wakati akichangia katika mkutano wa wakuu wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki unaojadili maendeleo na upatikanaji wa fedha kwa ajili ya miradi ya sekta ya miundombinu na afya.

Kabla ya Rais Magufuli kutoa mchango wake, Marais walioshiriki mkutano huo wamepokea taarifa ya mkutano wa majadiliano ya kisekta kuhusu mahitaji ya fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya sekta ya miundombinu na afya ambapo imeelezwa kuwa katika miaka 10 ijayo nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zitahitaji Dola za Marekani Bilioni 78 kutekeleza miradi ya miundombinu inayopendekezwa.

Katika mchango wake Rais Magufuli amesema pamoja na kutumia mfumo wa PPP ni muhimu kwa Serikali za kila nchi kusimamia vizuri ukusanyaji wa mapato ya kodi na rasilimali nyingine ili kutekeleza miradi ya miundombinu, afya na sekta nyingine.

Marais waliohudhuria mkutano huo ni Rais wa Uganda, Yoweri Kaguta Museveni, Rais wa Kenya, Uhuru Muigai Kenyatta, Rais wa Sudan Kusini,Salva Kiir Mayardit na Marais wa Rwanda na Burundi wamewakilishwa.