Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kimeponda kauli ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ya kusimamisha shughuli za mabaraza ya kata na kuingilia utendaji kazi wa mahakama.
Kimesema kuwakusanya wananchi kusikiliza kero zao za ardhi maana yake ni kutatua kero hizo bila sheria.
Akizungumza leo Februari 13, 2018 wakati akitoa tamko dhidi ya ukiukwaji wa utawala wa sheria, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Felista Mauya amesema watendaji wa Serikali wanapaswa kuheshimu utaratibu wa utendaji kazi, kuacha kuingilia majukumu ya taasisi na mihimili mingine.
Huku akinukuu alichokisema Makonda Februari 10, 2018 jijini Dar es Salaam, Mauya amesema, “ Makonda alisema ‘mahakama haitaki kuguswa kwa kisingizio cha mhimili mwingine, wamechukua nafasi ya Mungu na mimi ni mteule wa Mungu lazima niwaseme’. Huku ni kushambulia utendaji wa mahakama kinyume cha Katiba aliyoapa kuilinda.”
Februari 10, 2018 Makonda alipokea ripoti kutoka kwa wanasheria waliosikiliza kero za wananchi kwa uratibu wa ofisi yake.
Katika mkutano huo, mkuu huyo wa mkoa aliwaita jukwaa kuu wakuu wa idara ya ardhi na nyinginezo kutoka manispaa zote tano za Dar es Salaam na kuwahoji kuhusu idadi ya migogoro na changamoto katika maeneo yao ya kazi.
Katika maelezo yake ya leo, Mauya amesema ibara ya 107A ya Katiba inasema mamlaka yenye kauli ya mwisho ya utoaji haki Tanzania itakuwa mahakama.
“Wakati huohuo Ibara ya 107B inasisitiza uhuru wa mahakama katika utekelezaji wa majukumu yake. Kwa hiyo kwa mujibu wa ibara hii mihimili mingine ya dola na watendaji wake hawapaswi kwa namna yoyote ile kuingilia utendaji wa mahakama,” amesema Mauya.
Amebainisha kuwa kituo hicho kinawakumbusha viongozi wa Serikali na wanasiasa kuwa hawana mamlaka kisheria kuingilia utendaji kazi wa chombo hicho wala kuelekeza utendaji, badala yake wanapaswa kuheshimu na kufuata taratibu katika upatikanaji wa haki.
“Tumebaini mkutano wa mkuu huyo wa mkoa na wananchi wa jiji lake kulikuwa na mapungufu kadhaa ambayo yamekuwa yakifanywa na sio tu na Makonda, bali pia na baadhi ya viongozi wengine wa Serikali,” amesema.
Amesema sheria ya utatuzi ya migogoro ya ardhi inamtaja waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuwa na mamlaka juu ya mabaraza ya ardhi ya kata.
“Kifungu cha 10(1) cha sheria ya utatuzi wa migogoro ya ardhi namba 216 ya mwaka 2002 kinayatambua mabaraza ya kata kama mahakama ya utatuzi wa migogoro ya ardhi kwa ngazi ya kata, hivyo kwa mujibu wa sheria hizi wakuu wa mikoa hawana mamlaka ya kusimamisha, kuendesha wala kuelekeza utendaji,” ameongeza Mauya.
Kwa upande wake, Mkurugezi wa Utetezi na Maboresho wa LHRC, Anna Henga amesema lengo la tamko hilo ni kutaka umma ufahamu kuwa kitendo cha wakuu wa mikoa kuingilia mahakama si sahihi.
Amesema pia wametoa tamko hilo ili wananchi waelimike na kutambua kuwa ili kufikia haki kuna utaratibu umewekwa kisheria.
“Kwanza wajue ni utaratibu upi uliopo kisheria kwani kuna mahakama kitengo cha ardhi, mabaraza ya kata lakini tukisema tuwakusanye kila mmoja aeleze shida yake tutakuwa tunatatua kero bila sheria,” amesema.