SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Ijumaa, 8 Desemba 2017

T media news

JE NABII ISA, MWANA WA MARYAM, AKIRUDI DUNIANI ATAFANYA NINI, NA ATATAMBULIKA VIPI?

JIBU

BISMILLAH
Ujio wa Namii Isa, mwana wa Maryam ni mojawapo wa misingi ya Itikadi ya ‎Uwislamu. Ujio huo umetajwa na Qur’ani na Hadithi za Mtume ‎ﷺ‎ .  Tuanze ‎na baadhi ya Aya za Qur’ani zenye kuzungumzia suala hilo, na kisha ‎tugeukie Hadithi za Mtume ‎ﷺ‎ .‎
Mwenyezi Mungu ‎سبحانه وتعالى‎ anasema: Kwenye Surat An-Nisaa, Aya ‎nambari 157 hadi 159:‎
وَقَوْلِهِمْ إِنَّا قَتَلْنَا الْمَسِيحَ عِيسَى ابْنَ مَرْيَمَ رَسُولَ اللَّهِ وَمَا قَتَلُوهُ وَمَا صَلَبُوهُ وَلَٰكِن شُبِّهَ لَهُمْ ۚ وَإِنَّ الَّذِينَ ‏اخْتَلَفُوا فِيهِ لَفِي شَكٍّ مِّنْهُ ۚ مَا لَهُم بِهِ مِنْ عِلْمٍ إِلَّا اتِّبَاعَ الظَّنِّ ۚ وَمَا قَتَلُوهُ يَقِينًا (157) بَل رَّفَعَهُ اللَّهُ إِلَيْهِ ۚ ‏وَكَانَ اللَّهُ عَزِيزًا حَكِيمًا (158) وَإِن مِّنْ أَهْلِ الْكِتَابِ إِلَّا لَيُؤْمِنَنَّ بِهِ قَبْلَ مَوْتِهِ ۖ وَيَوْمَ الْقِيَامَةِ يَكُونُ عَلَيْهِمْ ‏شَهِيدًا (159 )‏‎ ‎
‎ “Na kwa kusema kwao: “Sisi tumemuua Masihi Isa, mwana wa Maryam; ‎Mtjme wa Mwenyezi Mungu” – nao hawakumuua wala hawakumsulubu, bali ‎walifananishiwa naye, tu. Na hakika wenye kuzozana/kubishana katika haya ‎wamo katika shaka nayo (wenyewe hawaamini). Wao hawana ujuzi nayo ‎wowote, ila kufuata udhanifu tu. Na hawana uyakini wa kumuua. Bali ‎Mwenyezi Mungu alimpandisha Kwake, na hakika Mwneyezi Mungu ni ‎Mwenye nguvu, Mwenye hekima. Na hawi katika Watu wa Kitabu ila hakika ‎atamuamini yeye kabla ya kufa kwake. Na Siku ya Kiyama atakua shahidi juu ‎yao.”  (An-Nisaa: 157-59.)‎

Hadithi zipo nyingi. Zifuatazo, hata hivyo, zitatosha kufafanua.‎

‏1. عن أبي هريرة رضي الله عنه أن النبي صلى الله عليه وسلم قال:" والذي نفسي بيده ليوشكن أن ‏ينزل فيكم ابن مريم حكما عادلا , فيكسر الصليب , ويقتل الخنزير, ويضع الجزية ,لا يقبل من كافر ‏‏,ويفيض المال حتى لا يقبله أحد, حتى تكون السجدة الواحدة خير من الدنيا وما فيها." (متفق عليه )‏‎ ‎
Imepokewa kutoka kwa Abu Hurayra ‎رضي الله عنه‎ akisema: Amesema Mtume ‎ﷺ‎ : “Naapa kwa Yule Ambaye nafsi yangu imo mikononi Mwake: Wakati ‎wowote anaweza kuteremshwa Mwana  wa Maryam, muamuzi mwadilifu, ‎kuja kuvunja misalaba, na kuua nguruwe, na kuweka sharia ya kodi za ‎kichwa (kwa wasioamini Upweke wa Mwwenyezi Mungu); hatokubali ‎kupokea mali kutoka kwa kafiri, na atagawa mali mpaka ifike hadi kuwa ‎hakuna mtu wa kuipokea, na kufika hadi kuwa kusujudu sijda moja  (ie ‎kumuabudu Mwenyezi Mungu) ndiyo bora zaidi kuliko dunia na kila ‎kilichomo ndani yake.” Muttafaq Alayhi.‎

Riwaya nyengine inasema:  ‎
وفي رواية: والله لينزلن ابن مريم حكما عادلا ,فليكسرن الصليب , وليقتلن الخنزير, وليضعن الجزية, ‏ولتتركن القلاص فلا يسعى عليها , وولتذهبن الشحناء والتباغض والتحاسد ,وليدعون إلى المال فلا ‏يقبله أحد (رواه مسلم )‏
‎“Naapa atateremshwa Mwana wa  Maryam; muamuzi muadilifu, kuja kuvunja ‎misalaba, kuua nguruwe, kuweka sharia ya kodi ya jizya, na itafika hadi ‎kukimbiwa kinda  jike la ngamia (yaani viumbe havitashughulishwa na ‎mambo ya kidunia); utatoweka uhasama, bughudha na kuhusudiana ‎‎(wanadamu wataacha kuhasimiana, kugombana, kubughudhin, kuhusudiana) ‎na ataita watu awape mali lakini hakuna atayekubali kuipokea ‎‎(wameshughulishwa na mamabo ya Akhera tu).” Ameipokea Muslim. ‎
‎ ‎
‏2 .عن حذيفة بن أسيد رضي الله عنه قال :اطلع النبي صلى الله عليه وسلم علينا ونحن نتذاكر الساعة ‏‏,فقال :" ما تذكرون؟" قلنا: نذكر الساعة.قال: " انها لن تقوم حتى ترو قبلها عشر آيات: الدخان,والدابة ‏‏. وطلوع الشمس من مغربها, ونزول عيسى ابن مريم, ويأجوج ومأجوج, وثلاثة خسوف: خسف ‏بالمشرق ,و خسف بالمغرب, وخسف بجزيرة العرب, وآخر ذلك نار تخرج من قبل عدن -في اليمن – ‏تطرد الناس إلى محشرهم (رواه مسلم )‏
‎2. Imepokewa kutoka kwa  Hudhayfa bin Usayd ‎رضي الله عنه‎  akisema: ‎Alitushtukia Mtume ‎ﷺ‎ wakati sisi tukuwa tunazungumza na kukumbushana ‎kuhusu ujio wa Kiyaa. Basi akatuuliza: “Mnazungumza nini?”  Tukasema: ‎‎“Tunakumbushana kuhusu ujio wa Kiyama!” Basi akasema kutuambi: ‎
‎“Hakitasimama Kiyama mpaka muone dalili kumi. 1. Moshi (mioto ya visima ‎vya mafuta?), 2. Mnyama (atayesema); 3. Jua kuchomoza machweo yake; 4. ‎Kuteremka duniani Isa mwana wa Maryam, 5. Kutokeza Yaajuju wa Majuju; ‎‎6. Kupatwa kwa mwezi (wakati mmoja) maeneo matatu: 7.Mashariki (Asia), ‎‎8. Magharibi (Ulaya) na 9. Bara Arabu (Mashariki ya Kati),  na mwisho wa ‎yote hayo, 10 . Moto utaotokea upande wa Aden –ndani ya Yaman-  ‎utaowaswaga  wanaadamu kuelekea watapofufuliwa.” Ameipokea Muslim. ‎

Ama kuhusu dalili za ujio wa Nabii Issa – na  ndiyo kiini cha suala lako- ‎msikilize Mtume ‎ﷺ‎ anasema nini kuhusu hayo:‎

‎ 1817. Imepokewa kutoka kwa al-Nawaas bin Sam’aan ‎رضي الله عنه‎ akisema: ‎Siku moja asubuhi, Mtume ‎ﷺ‎ alimtaja Dajjali kwa kumuelezea ni nani yeye. ‎Basi, alimbeza, kwa upande mmoja, na akamvuvumisha (tunisha), kwa ‎upande wa pili, mpaka tukaingiwa na khofu kwa kudhani kwamba hayupo ‎mbali nasi, amejificha tu, karibu nasi, kwenye chaka la mitende. ‎

Jioni yake, tulirudi kwa Mtume ‎ﷺ‎ na alipotuona tu aling’amua kuwa ‎tumejawa na kiherehere (hofu na woga). ‎

Basi akasema: “Mna wasi wasi wa nini?” ‎

Tukamjibu: “Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu! Hii leo asubuhi umemuelezea ‎Dajjali, ukamdharau kwa upande mmoja, lakini kwa upande wa pili ulimtunisha ‎vile vile, tukaingiwa na hofu kwa kudhani kwamba hayupo mbali nasi, ‎amejificha tu, kwenye chaka la mitende!” Basi Mtume ‎ﷺ‎ akasema: ‎

‎“Ninacho wacheleeni zaidi, si Dajjali! Maana akitokea na mimi niko hai pamoja ‎nanyi, mimi ndiye nitayepambana naye! Siyo nyinyi! Na endapo atatokea, ‎wakati mimi siko nanyi duniani, basi hapo ndipo kila mtu atapambana naye ‎mwenyewe! Na Mwenyezi Mungu, pekee, Ndiye ninayemuacha kuwa Mlinzi ‎wa kila Mwislamu.‎

Dajjali ni kijana mwenye nywele zilizo songasonga sana, chongo jicho ‎moja, namfananisha, kwa sura, na ‘Abdil’uzza bin Qatwan. Atayekutana naye, ‎minongoni mwenu, amsomee Aya za mwanzo za Surat al-Kahf. Atazuka katika ‎eneo liliopo baina ya Shaam (Syria) na Iraq, akibeba upanga (silaha) na ‎kumwaga damu, kulia na kushoto (ISIS!??)! Hivyo, Enyi waja wa Mwenyezi ‎Mungu! Msiyumbishwe! Kuweni imara! ‎

Tukasema, kumuuliza: “Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu! Ataishi kwa ‎muda gani duniani?” Akajibu kwa kusema: “Siku arubaini. Moja katika siku ‎zake, itafanana na mwaka mmoja, na moja itafanana na mwezi mmoja, na moja ‎itafanana na juma moja, na siku zake ziliosalia zitafanana na siku zenu nyinyi.”‎

Tukasema: “Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu! Je, ile siku yake moja ‎yenye kufanana na mwaka mmoja, swala zetu tano, za kila siku, itatosha ‎kuziswali kama tunavyoziswali?” Akajibu: “Hapana! Mtaziswali kuendana na ‎muda wa siku yake!”‎

Tukasema: “Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu! Atakuwa na kasi ‎‎(nguvu) za aina gani, duniani?”  Akajibu: “Kama kasi ya wingu linalosukumwa ‎na upepo mkali. Atawaendea watu na kuwalingania wamfuate, na wao ‎watamfuata na kumuamini. Ataamrisha mawingu yanyeshe mvua,  na mvua ‎itanyesha. Ataiamuru ardhi ioteshe miti na mimea, na ardhi itaotesha miti na ‎mimea. Mifugo yao itarudi jioni ikiwa imenona, tipwatipwa; matiti yao yamejaa ‎maziwa zaidi na mbavu zao na mapaja yao yamenenepa zaidi! ‎

Kisha atawaendea watu wengine na kuwalingania wamfuate, lakini ‎watamkatalia. Hivyo, atawaacha na kwenda zake. Wataanza kukumbwa na ‎ukame na kupoteza mali zao, hadi kusambaa njaa miongoni mwao. ‎

Atapita jangwani kwenye maeneo yaliyo makame zaidi, na kuyaambia ‎yacheue hazine zake; na hazina zitatoka nje na kumfuata nyuma, kama kundi la ‎nyuki.‎
‎ ‎
Kisha atamwita mvulana, shababi, aende mbele yake. Akimfikia atamkata ‎kwa upanga pande mbili, na kuzirusha mbali mrusho wa mshale kwenda ‎kwenye shabaha yake. Kisha atamwita arudi kwake. Basi atamrudia kwa uso wa ‎bashasha na vicheko.‎

Vile akiwa katika mazingaombwe yake hayo, Mwenyezi Mungu ‎سبحانه ‏وتعالي‎ Atamteremsha Masihi Isa mwana wa Maryam, karibu na mnara mweupe, ‎mashariki ya mji wa Dimashk, akiwa amevaa nguo mbili zenye rangi ya ‎zaafarani (njano iliyokoza), huku ameegesha mikono yake miwili juu ya mbawa ‎za Malaika wawili. Akiinamisha chini kichwa chake basi hutoja maji yanayo ‎ng’aa kama fedha, na anapoinua kichwa chake hutoja matone ya maji mfano wa ‎lulu. Kafiri, yeyote, atayeguswa na pumzi zake atafariki papo hapo. Na pumzi ‎zake huishia pale linapoishia kuona jicho lake. ‎

Isa mwana wa Maryam atamsaka Dajjal kila upande mpaka atakutana ‎naye kwenye kijiji cha Ludd, na papo hapo atamchinja!‎

Kisha, Isa mwana wa Maryam, atawatembelea watu waliohifadhiwa na ‎Mwenyezi Mungu kutokana na fitina za Dajjal,  na kuzipangusa (vumbi) nyuso ‎zao, na kuwatajia nafasi za vyeo vyao Peponi. Vile akiwa katika shughuli yake ‎hiyo, Mwenyezi Mungu ‎سبحانه وتعالي‎ Atamteremshia Wahy (Ufunuo kutoka ‎mbinguni) kumuambia: “Nimeumba waja wangu, ambao hapana mtu yeyote ‎anayeweza kupigana nao au kuwashnda. Hivyo basi, waongoze waja Wangu ‎kuelekea Mlima Siina (Sina).” ‎

Hapo Mwenyezi Mungu Atawafungulia Juju-wa-Majuju wataotiririka ‎kutoka kila mlima na kutapakaa kila upande (al-Anbiyaa:96). Kundi lao, moja, ‎liliotangulia litapita kando kando ya Bwawa Tabariyya na kuyanywa maji yake ‎yote. Pale kundi lao la mwisho litapofika katika eneo la Bwawa hilo, watasema: ‎‎“Wakati mmoja, palikuwepo maji hapa!” Hapo, Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, ‎Isa bin Maryam na wafuasi wake, watazingirwa na kuwa katika hali ngumu ‎mpaka watafika hadi kuona kuwa kichwa cha ng’ombe, kwa wao, ni afadhali ‎zaidi kuliko dinari mia moja, mnavyo ziona nyinyi hii leo kuwa ni bora zaidi. ‎

‎ Hapo, Mtume wa Mwenyezi Mungu, Isa mwana wa Maryam, pamoja na ‎wafuasi wake, watamuomba Mwenyezi Mungu Awasaidie kupambana na Juju-‎wa-Majuj. Basi Mwenyezi Mungu ‎سبحانه وتعالي‎ Atawateremshia virusi vya ‎maradhi kwenye shingo zao, ambavyo vitawaua wote, kwa pamoja, siku moja, ‎wakati mmoja.‎

Kisha, atateremka, kutoka Mlima Sina, Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, ‎Isa mwana wa Maryam, akifuatwa na watu wake. Lakini wakifika chini ‎hawatakuta nafasi ya hata nchi moja kwenye ardhi, kwa vile imejaa mizoga ya ‎Juju-wa-Majuju na kutapakaa harufu ya uozo wao. ‎

Hapo, Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, Isa mwana wa Maryam, pamoja na ‎wafuasi wake, watamuomba Mwenyezi Mungu Awasaidie. Basi Mwenyezi ‎Mungu ‎سبحانه وتعالي‎ Atawateremshia ndege wakubwa wenye shingo ndefu, kama ‎shingo za ngamia, wataochukua mizoga hiyo na kuipeleka Alikowatuma ‎Mwenyezi Mungu. ‎

Kisha Atateremsha Mwenyezi Mungu, mvua kubwa sana itayoosha na ‎kusafisha kila jengo, liwe la udongo, mawe, au manyoya (mahema), na hivyo ‎kuonekana kuwa safi kabisa kama kioo. ‎

Kisha dunia itaamrishwa na Mwenyezi Mungu, ioteshe matunda yake na ‎kurudisha baraka (neema) zake, kiasi kwamba komamanga moja litaweza ‎kuwalisha kundi kubwa la watu, na wataweza kukaa kwa pamoja chini ya kivuli ‎cha jani lake moja. ‎

Mifugo nayo itabarikiwa kiasi kwamba maziwa ya ngamia mmoja ‎yanaweza kutosha kulisha kundi kubwa la watu, na maziwa ya ng’ombe mmoja ‎yataweza kulisha jamii nzima ya kabila moja, na maziwa ya mbuzi mmoja ‎yanaweza kulisha familia moja. ‎

Vile watu wakiwa katika hali hiyo, Mwenyezi Mungu Atawatumia upepo ‎mwanana, utaovuma chini ya kwapa zao, na kuchukua roho ya kila mwenye ‎kuamini na kila Mwislamu, na kusalia watu waovu, wenye kufanya ngono ‎kadmnasi, bila ya kuona haya wala kuona vibaya, kama wanavyo fanya ‎punda. Ni juu ya watu hao, ndio Kiyama kitawashukia!”  Ameipokea Muslim.‎

والله أعلم

وبالله التوفيق

السيد عبد القادر شريف آل الشيخ أبى بكر بن سالم‎ ‎

Imejbiwa na Sayyid Abdulqadir Shareef

NI RUHUSA KUNUKUU, kama ilivyo, pasi na kubadilisha au kuongeza ‎chchote, na kuweka kwenye FB yako au kwenye ‎WhatsApp na kwenye ‎Makundi ya Mitandao ya Kijamii za Kiislamu, ‎kwa lengo la kusambaza na ‎kuelimisha Dini. Changia kusambaza ‎Dini, ujipatie thawabu.‎

kcwajawema@gmail.com