Nimepata nafasi ya kumsikiliza Mh Tundu Lissu alipozungumzia suala la la ndege ya bombardia ambayo serikali ya Tanzania inailipia ili iinunue kule nchini Kanada. Lakini kwanza ninaona ni vyema nieleze matabaka ambayo yanaweza kujengeka kwenye jamii kabla ya kutoa maoni yangu kuhusu suala hili.
Wataalam wa sayansi ya jamii wanasema, kutokana na unyonyaji au uporaji wa uchumi ambao unaweza kufanywa kwa njia mbalimbali za kifisadi na kikundi cha watu husababisha kujengeka kwa matabaka katika jamii. Tabaka la kwanza ni la matajiri ambalo humilki sehemu kubwa ya uchumi wa nchi kwa njia ya ufisadi au unyonyaji. Kwa lugha ya kigiriki, tabaka hili linaitwa origarchy (oligaki).
Oligaki huweka rais wao madarakani ili waweze waweze kuendelea kupora utajiri kwa kumtumia rais waliyemweka madarakani. Oligaki wataweka majaji wao kwenye mhimili wa mahakama ili wakiwa na kesi waweze kushinda. Oligaki wataweka watu wao kwenye vyombo vya usalama, wataweka wabunge na madiwani wao ili maamuzi yatakayopitishwa yaweze kuwanufaisha wao.
Kuwepo kwa tabaka hili husababisha kuwepo na matumizi makubwa ya fedha kwenye chaguzi. Oligaki hutumia fedha nyingi kuwanunua watu ili wawapitishe wagombea wao kwenye chaguzi hizo. Wagombea wanaofadhiliwa na oligaki hupita makanisani, misikitini na kwenye jamii wakitoa misaada mbali mbali ili wapate kukubalika hatimae wachaguliwe. Lakini baada ya kuchaguliwa hutetea maslahi ya oligaki badala ya maslahi ya wananchi.
Tabaka la pili ni lile la marafiki au ndugu wa oligaki. Tabaka hili huitwa aristrocracy (asistrokasi). Aristrokasi ni watu waliowekwa na origaki ambao wapo kwenye taasisi za fedha, ubalozi, serikalini, na vyama vya siasa. Tabaka hili kazi yake ni kutetea na kulinda maslahi ya mafisadi ambao hutafuta kushika au wameshika njia kuu za uchumi za nchi na hivyo tabaka hili huwa na upinzani mkubwa na serikali na kwenye bunge kwa lengo lakutetea maslahi ya matajiri. Aidha, tabaka hili hujivika ngozi ya kondoo, kwa kujiita watetezi wa watu wanyonge.
Tabaka la tatu ni la watu wenye tamaa ya madaraka, tabaka hili huitwa timocracy (timokrasi). Watu walioko kwenye tabaka hili huunga mkono hoja za oligaki na aristrokasi na hutamani siku moja waingie kwenye matabaka hayo. Timokrasi ni watu wasio na msimamo wowote, kwani wametawaliwa na tamaa na makuu na kiburi na ubinafsi. Timokrasi ni wepesi kuwasaliti wananchi. Hawana chembe ya uzalendo kwa nchi yao. Timokrasi ni wanafiki. Na mnafiki humtukuza yeyote, kwa lolote, kwa matumaini ya chochote; ndivyo walivyo.
Tabaka la nne ni la wanachi maskini wanaotegemea maisha bora kutoka kwenye serikali walioichagua.
Matabaka haya yamejengeka kwa kasi sana hapa nchini kuanzia mwishoni mwa utawala wa rais Mkapa. Kutokana na kuwepo kwa matabaka haya watanzania masikini waliendelea kushuhudia utajiri wan chi hii ukiwanufaisha watu wachache walioko kwenye matabaka ya oligaki,aristrokasi na timokrasi. Serikali ya awamu ya tano imeonyesha dhamira ya kweli ya kuhakikisha rasilimali za nchi hii zinawanufaisha watu watanzania wote. Lakini ni dhahiri pia kwamba tabaka la oligaki, aristrokasi na timokrasi hawafurahishwi na jitihada za serikali hivyo wanapambanma kuhakikisha juhudi za serikali hazifanikiwi. Ni dhahiri nchi yetu iko kwenye vita ya uchumi. Vita hii ni ngumu sana kupita vita ya kupigania uhuru. Katika vita hii ya uchumi, wapo watanzania watakaogeuka mawe na kuwa wasaliti wakiungana na oligaki lakini wakijificha kwa kuvaa ngozi ya kondoo, wakijifanya ni watetezi wa watanzania maskini wakati ni watetezi wa mafisadi(oligaki).
Hivi Karibuni nilipata nafasi ya kumsikiliza Mheshimiwa Tundu Antipas Lissu mbunge wa jimbo la Singida Mashariki alipokuwa akichangia kuhusu suala la hatua ambazo zimechukuliwa na seriklai kuhusu makinikia au mabaki ya mchanga kutoka kwenye migodi ya dhahabu. Kwa upande wangu nilimuona alitumia lugha kali sana na alikuwa na ghadhabu. Nilijiuliza sana kuhusu mchango alioutoa na ghadhabu alizoonyesha. Imebidi nijaribu kufuatilia misismamo yake, huu ni mtazamo wangu tu.
Mwaka 2015 wakati Lowassa anahamia Chadema kutoka CCM nilipata taabu kubwa nilipomwona Tundu Lissu akiwa ndiye alikuwa akimtetea Lowassa kuhamia Chadema na akimlaumu Dk Slaa.
Wakati wa kampeni 2015 UKAWA ilikuwa na kazi ngumu kuwashawishi watanzania kuhusu suala la ufisadi. Ajenda ya ufisadi ikafa. Uchaguzi ukafanyika, watanzania wakaamua waendelee kuongozwa na CCM. CCM ikaunda serikali.
Serikali ya CCM chini ya uongozi wa John Pombe Magufuli (JPM) ikaanza kushughulikia suala la ubadhirifu, uzembe, na maadili kwa watumishi wa umma. Watumishi wengi walichukuliwa hatua kali na serikali ya CCM chini ya uongozi wa JPM. Mtakumbuka, kuna kiongozi a;liyekuwa analipwa mishahara 17. Mtakumbuka uozo kwenye bandari ya Dar es salaam. Na mtakumbuka kwamba walipatikana wafanya kazi hewa zaidi ya elfu 10, wanafunzi hewa na suala la madawa ya kulevya.
Tundu Lissu na Chadema walilalamika juu ya hatua zilizochukuliwa na serikali, wakisema watu hao waliochukuliwa hatua wanaonewa au utaratibu uliotumika ni mbovu. Mashaka yangu juu ya Mheshimiwa Tundu Lissu yakazidi kuwa makubwa.
Lakini pia mtakumbuka kuhusu suala la UKUTA. Wabunge wa UKAWA walikuwa wakifunga midomo wakiwa bungeni wakidai demokrasia pana. Lakini kwa sasa ni dhahiri kwa watu wengi kuwa ndani ya CCM kuna demokrasia pana kuliko ndani ya Chadema. Hili limedhibitishwa na uchaguzi wa wabunge wa bunge la Afrika Mashariki. CCM ilifanya mchakato wa kidemokrasia kuwapata wabunge wa Afrika Mashariki kuliko ilivyokuwa ndani ya Chadema. Haya yote yaliyofanyika ndani ya Chadema Lissu akiwemo na ni mwanasheria Mkuu wa Chadema. Ninaanza kujiridhisha kwamba Mheshimiwa Tundu Lissu siye niliyemfahamu.
Rais John Pombe Magufuli amedhubutu kuchukua hatua juu ya upotevu wa mapato yaliyotokana na kupelekwa makinikia nje ya nchi na kuagiza uchunguzi ufanyike. Ripoti ya uchunguzi imefichua ufisadi wa kutisha kwenye usafirishaji wa makinikia nje ya nchi. Watanzania wengi wazalendo waliosikiliza ripoti hiyo wameumia sana kwa taarifa zilizomo kwenye ripoti hiyo. Watanzania tumenyonywa kiasi cha kutosha.
Mliopata nafasi ya kumsikiliza Mheshimiwa Tundu Antipas Lissu, amesema Rais amefanya jambo la hovyo sana. Na alionekana kukasirika sana. Hiki kimenishitua sana na ninashawishika kuamini kwamba Lissu hayuko sawa, ana ulemavu usioonekana kwa macho. Tundu Lissu ni mwanasheria mzuri sana lakini amekosa roho ya kuipenda nchi yake, amekosa chembe ya roho ya uzalendo.
Nina amini vyama vya siasa vinatakiwa kuungana katika masuala ambayo yana maslahi mapana kitaifa kama hili suala la makinikia kupelekwa nje ya nchi. Aidha, wataalamu wanatakiwa kujitokeza kutoa ushauri namna ya kuboresha ripoti iliyotolewa na kuisaidia serikali ili iweze kuisaidia serikali kuchukua hatua sitahiki. Lakini Tundu Lissu alikebehi au kudhihaki hatua ikliyochukuliwa na serikali.
Wapo watanzania wengi waliomwamini sana Tundu Lissu na wanataabika na misimamo yake ya hivi karibuni kama ninavyotaabika mimi.
Serikali ya awamu ya tano imefanya utaratibu wa kununua ndege kutoka Canada kwa lengo la kuboresha usafiri wa anga na kuinua utalii nchini. Bila shaka watanzania wengi wanaunga mkono jitihada hizi za serikali kwani ilikuwa ni aibu kwa nchi yetu ilipokuwa haina ndege hata moja.
Siku chache zilizopita, Mh Tundu Lissu ameeleza kuwa ndege aina ya bombardier mali ya serikali ya Tanzania imeshikiliwa huko Kanada na kampuni moja ya ujenzi kutokana na kuidai serikali ya Tanzania. Iwe ni kweli au siyo kweli hoja yangu siyo hiyo. Kinachoendelea kunitaabisha ni kwa nini Mh Tundu Lissu anaonekana kufurahia nchi kupata tatizo hili na matatizo mengine yaliyopita. Haonyeshi kusononeshwa nchi yake inapopata matatizo au misukosuko. Nchi inapopata matatizo au misukosuko Mh Lissu huchekelea. Mtakumbuka serikali ilipochukua hatua dhidi ya ubadhirifu kwenye halmashauri Mh Lissu alisema wafanyakazi waliotumbuliwa walionewa na alisema atawatetea mahakamani, kwenye suala la makinikia Mh Lissu alisema Rais amefanya maamuzi ya hovyo sana na serikali itashitakiwa. Juzi Mh Tundu Lissu alionekana kufurahia ndege ya bombardier kushikiliwa na Kanada. Mh Lissu ni mbunge angeweza kuishauri serikali akiwa bungeni lakini ameona ni vizuri kwake kuidhalilisha serikali kwenye vyombo vya habari.
Mh Lissu haoni kabisa nia njema ya serikali ya kununua ndege ili kuboresha usafiri wa anga nchini. Mh Lissu haoni kabisa nia njema ya serikali kuhakikisha madini yetu yanawanufaisha watanzania, mh Lissu haoni kabisa jitihada za serikali kupiga vita ubadhirifu kwa watumishi wa serikali na halmashauri zetu, Mh Tundu Lissu haoni kabisa jitihada za serikali kuboresha elimu na huduma za afya ? Ghadhabu za Mh Lissu zinatokana na nini hasa ? Au Mh Lissu ana mtetea nani katika hoja zake kama haoni jitihada za serikali zinazowalenga wanachi maskini ?
Je katika misimamo ambayo Mh Lissu ameionyesha kwenye suala la makinikia, suala la ununuzi wa ndege, anampigania au ana mtetea nani ? Nionyeshe marafiki wa Mh Tundu Lissu nami Nitakuonyesha Oligaki, Aristrokasi, na Timokrasi.
By Fred Mpendazoe