MSANII mkongwe wa filamu nchini, Jacob Steven ‘JB’ ametangaza kujiengua katika uigizaji na sasa ameanzisha Taasisi ya Barazani Entertainment ili kulinda heshima yake.
Katika mahojiano maalum katikati ya wiki hii, JB ambaye anachukuliwa kama mmoja wa waigizaji mahiri kuwahi kutokea, hajaondoka moja kwa moja katika filamu bali amebadili nafasi na sasa atakuwa msambazaji.
“Nimeshakuwa muigizaji na mtengenezaji na nimekuwa nikipeleka filamu zangu na wenzangu mahali palepale siku zote, halafu tunapanga foleni kusubiri kulipwa. Sasa unapofikia hatua kama hii, lazima utazame nje ya boksi.
“Naachana na filamu na kuwaachia vijana ili nitunze heshima yangu, maana nikiendelea, iko siku watanivunjia heshima ambayo nimeijenga kwa miaka mingi,” anasema JB.
“Wasanii tumejichangisha na kuunda taasisi iitwayo Barazani Entertainment, hii itahusika na usambazaji filamu kwa njia za kisasa zaidi. Ni mtandao unaohitaji muda, lakini nikuhakikishie kwamba haya ni mapinduzi makubwa katika filamu.
“Barazani Entertainments itaajiri kijana mmoja, ambaye sisi tutamuita venda, kwa kila nyumba 500 nchi nzima. Katika eneo hili, tunategemea kuwa ajili zaidi ya vijana 9000. Kazi yao itakuwa ni kusambaza filamu kwa haraka popote itakapohitajika.
“Kwa mfano, kama mtu anataka kununua filamu na yupo Chato, ndani ya saa moja filamu hiyo itakuwa barazani kwake, kwa sababu nyumba ya mteja huyo itakuwa miongoni mwa nyumba 500 za venda wetu. Ndiyo maana tunaitwa Barazani kwa sababu itakufikia hapo hapo ulipo.
“Kwa wasanii, kwanza hata kama wana wazo tu la filamu na hawana fedha, wakija kwetu na tukakubaliana na wazo lake, atatengenezewa filamu na kuiingiza sokoni halafu tutakatana zile gharama baada ya mauzo,” anasema JB.
Kuhusu kudorora kwa soko la filamu nchini, JB anasema: “Tatizo tasnia iliingiliwa, kila mtu anadhani anaweza kuwa msanii, mwongozaji au mtengeneza skripti, tulichodhamiria kukifanya ni kwamba tutasambaza filamu zenye ubora tu na hii tutausimamia wenyewe, tunataka tasnia irudi katika mstari ulionyooka.”