SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumapili, 6 Novemba 2016

T media news

Watu sita wamefariki mkoani Mara katika matukio mawili tofauti.

Watu sita wamefariki mkoani Mara katika matukio mawili tofauti huku mmoja Mwihitimu wa darasa la saba katika shule ya msingi Rwamkoma Wilaya ya Butiama Rosalina Thomas mwenye umri wa miaka wa 13 akiuawa kwa sababu za kulazimishwa kufanya mapenzi.

 kamanda wa polisi mkoani hapa kamishina mwandamizi msaidizi wa jeshi la polisi Ramadhani Ng’anzi,amesema tukio la kuuawa kwa mwihitimu huyo wa darasa la saba limetokea katika kijiji cha Rwamkoma kata ya Butiama wilaya ya Butiama mkoani mara

Kamanda  Ng’anzi amesema chanzo cha mauaji ni kijana aliyekuwa akifanya kazi ya kusaga nafaka katika mashine ya familia hiyo Magige Werema(25) kuingia katika tamaa za kumtaka mtoto huyo kimapenzi,hivyo alitumia nguvu kumwingilia kimwili wakati wazazi wa familia hiyo wakiwa wametoka.

Amesema baada ya kijana huyo kumaliza kufanya ubakaji,alimkata  mtoto huyo mapanga ya kichwani,bega la kulia na kiganja cha mkono wa kulia na kisha kukimbilia katika kisima cha maji ambacho alijidumbukiza na kuzama.

Amesema baada ya polisi kupata taarifa za tukio hilo walifika na kuuchukua mwili wa mwanafunzi,pamoja na kufanya jitihada za kuupata mwili wa kijana huyo uliokuwa umenasa katika tope la kisima.

Kamanda Ng’anzi amesema taarifa ya daktari ilionesha kuwa mwili wa mwanafunzi huyo kabla ya kuuawa uliingiliwa kimwili,hivyo ni wazi kuwa mtuhumiwa ambae nae pia ni marehemu alimbaka mwanafunzi huyo.

Katika tukio lingine kamanda amesema katika kijiji cha Masaunga kata ya Kisorya Wilayani Bunda, watu wanne,watoto wa familia moja ya Siajali Magoti walikufa kwa kupigwa radi iliyokuwa imeambatana na mvua ya upepo.

Ng’anzi alisema watoto hao walikuwa wamelala katika chumba kimoja,huku wazazi wakiwa katika chumba kingine,na kwamba radi hiyo ilipita dirishani wakati mvua ikinyesha.

Amewataja waliokufa kuwa ni James Siajali(14),Penina Siajali(9),Eliza  Siajali(8) na Mujo Siajali(6).