SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatano, 23 Novemba 2016

T media news

Serikali yaanza kutekeleza upimaji ardhi nchi nzima

SERIKALI imeanza kutekeleza mpango wa upimaji viwanja nchini kwa miaka 10 katika wilaya tatu za mkoani Morogoro na kutoa hati miliki za kimila 50,000.

Mpango huo wa kupanga, upimaji na kumilikisha ardhi umeanza katika wilaya za Malinyi, Ulanga na Kilombero kwa ufadhili wa Benki ya Dunia (WB) na nchi za Uingereza, Denmark na Sweden.

Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk Yamungu Kayandabila alisema hayo wakati wa mahojiano yaliyofanyika katika kipindi cha ‘Tunatekeleza’ kinachoandaliwa na Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) na kurushwa na Televisheni ya TBC1 juzi.

Alisema hatua hiyo itasaidia kuondoa migogoro ya ardhi kwa kuwa na matumizi bora ya ardhi. Alisema katika sehemu za mijini halmashauri zinasimamia upimaji huo ikiwemo mradi wa viwanja 20,000 ulioanza tangu mwaka 2003 na ule wa Pemba Mnazi na sehemu nyinginezo.

Alisema upimaji huo unafanyika kwa kutumia fedha za wizara kupitia Mfuko wa Upimaji Viwanja ambapo wanakopesha halmashauri zenye uhitaji na sasa wanasaidiwa na sekta binafsi. Alitaka halmashauri kusimamia upimaji viwanja unaofanywa na sekta binafsi kwa kutumia bei elekezi ya upimaji na siyo kufidia kwa kuchukua viwanja.

“Halmashauri zinatakiwa kusimamia utaratibu wa wizara katika upimaji ardhi unaofanywa na watu binafsi kulingana na maelekezo ya wizara ili kuondoa migogoro,” alisema na kuongeza kuwa zaidi ya asilimia 70 ya miji yote ni makazi holela ukiongozwa na Arusha kwa kuwa na makazi holela ya asilimia 70 wakati Singida imepangwa kwa asilimia nane pekee.

Alisema kwa mkoa wa Dar es Salaam, asilimia 70 hadi 74 haijapangwa hivyo wameanza upangaji katika wilaya ya Ubungo katika kata za Ubungo, Kimara na Saranga ambako viwanja 3,000 vitatambuliwa. Alisema upangaji huo utakuwa shirikishi na wananchi kukubali na kuchangia huku wakipewa hati na kutengeneza miundombinu muhimu.