SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatano, 17 Agosti 2016

T media news

Yanga Sc v Azam Fc: Yanga wana kikosi kizito....

MECHI ya kukata ‘utepe’ wa msimu mpya wa ligi kuu Bara 2016/17 na michuano ya FA itapigwa Jumatano hii. Kwa mara ya nne mfululizo timu za Yanga SC na Azam FC zitacheza katika game ya Ngao ya Jamii huku Yanga ikiwa imeshinda mara tatu mfululizo na Azam FC mara moja.

Yanga ilishinda 1-0 Agosti, 2013, ikashinda 3-0 Agosti, 2014 na mwaka uliopita walifanikiwa kushinda kwa mara ya tatu, safari hii ikiwa kwa changamoto ya mikwaju ya penalti 8-7 baada ya suluhu-tasa katika muda wa dakika 90′.

Mara zote hizo wameishinda Azam FC. Je, Yanga wataendeleza kuishinda Azam FC na kutwaa ‘ndoo’ hiyo kwa mara ya nne mfululizo?

Ni falsafa za Holland vs Spain

Kocha, Mholland, Hans van der Pluijm tayari amejidhihirisha ni kati ya wakufunzi bora wa kigeni waliopata kufundisha VPL. Ameshinda mataji mawili ya VPL, moja la Ngao ya Jamii na lingine moja la FA Cup.

Mataji yake yamekuja baada ya kuitengeneza timu aliyoitaka na kuisajili mwenyewe. Hans anapendelea timu yake ishambulie kwa kasi huku wakipasiana pasi fupi fupi. Anakwenda uwanjani akiwa na kikosi chake kamili.

Alimshinda Stewart Hall mwaka mmoja uliopita lakini sasa anakutana na Azam ikiwa na kocha mpya raia wa Hispania, Zeben Hernandez.

Zeben ameichukua timu yenye sura nyingi za wachezaji ambazo zilifanya kazi na Muingereza, Hall.  Katika game zake za kujipima uwezo kocha huyo amekuwa akiichezesha timu yake katika mfumo wa 4-4-2 na ule wa 4-3-3.

Yanga wana kikosi kizito

Juma Abdul hatakuwapo lakini beki wao waliyemsajili kutoka simba Hassan Kessy ameruhusiwa kucheza katika mchezo huo, ‘kiraka’ Mbuyu Twite pia anaweza kurudi katika beki namba mbili. Mwinyi Haji baada ya kiwango cha juu dhidi ya MO Bejaia wikendi iliyopita atapangwa upande wa beki 3.

Nahodha, Nadir Haroub atarudi kikosini kucheza na Mtogo, Vicent Bossou katika beki ya kati. Hans atakuwa na beki ngumu huku safu ya kiungo ikitaraji kuongozwa na Mzimbabwe, Thaban Kamusoko, Said Juma Makapu, Saimon Msuva, Mnyarwanda, Haruna Niyonzima na Deus Kaseke.

Washambuliaji, Donald Ngoma raia wa Zimbabwe na Mrundi, Amis Tambwe wanataraji kuongoza safu ya mashambulizi. Hiki ni kikosi kikali na cha muda mrefu ambacho kitaendelea kuwasumbua Azam FC.

Kukosekana kwa mshambulizi raia wa Ivory Coast, Kipre Tchetche kunaweza kupunga makali ya safu ya mashambulizi ya Azam lakini bado, Hernandez anaweza kuwatumia, nahodha wake John Bocco, kijana, Farid Musa, Ramadhani Singano katika safu ya ushambuliaji.

Himid Mao, Muivory Coast, Kipre Bolou, Mnyarwanda, Jean Mugiraneza, Salum Abubakary wanaweza kuanza katika safu ya kiungo. Erasto Nyoni, Shomari Kapombe wanaweza kuanzishwa katika beki za pembeni.

Aggrey Morris na David Mwantika pia wanaweza kuanzishwa katika beki ya kati. Hiki ni kikosi bora pia tena kimecheza pamoja kwa muda mrefu sasa.

Tofauti inaweza kuletwa na timu ambayo wachezaji wake watakimbia uwanjani, watamiliki mpira, kuwa na ustahimilivu.

Yanga wako vizuri zaidi katika mambo hayo niliyoyataja lakini Azam nao wamekuwa na maandalizi ya muda mrefu. Nidhamu ya mchezo inaweza kuwabeba Yanga na kupata matokeo, vinginevyo inaweza kuwa game ndefu na mikwaju ya penati kuamua mshindi.