Yanga imeendelea kuandamwa na jinamizi la kukosa ushindi kwenye mechin zake baada ya leo Jumamosi August 6 kulazimishwa sare ya bila kufungana kwenye mchezon wa kirafiki wa kujipima nguvu dhidi ya Mtibwa Sugar uliochezwa kwenye uwanja wa taifa.
Kikosi cha Yanga haijapata ushindi katika mechi zake tano za mwisho, mechi ya mwisho waliyopata ushindi ilikuwa ni dhidi ya Azam mchezo wa fainali ya kombe la FA iliyopigwa May 25 mwaka huu.
Baada ya ushindi dhidi ya Azam, Yanga ilifungwa bao 1-0 ugenini na MO Bejaia, ikafungwa tena bao 1-0 nyumbani na TP Mazembe, ikatoka sare ya goli 1-1 na Medeama nyumbani kabla ya kufungwa magoli 3-1 ugenini. Mchezo wa leo dhidi ya Mtibwa unakamilisha idadi ya mechi 5 swa na dakika 450 bila ushindi wakati huo ikiwa imeruhusu kufungwa magoli 6 yenyewe ikifunga magoli mawili pekee.
Mchezo wa leo ulikuwa na lengo la kupima wachezaji kwa timu zote mbili ulikuwa ni wa kuvutia japo timu zote mbili zilishindwa kupata magoli.
Yanga wanajiandaa kwa ajili ya mchezo wao wa kombe la shirikisho dhidi ya MO Bejaia unaotarajiwa kuchezwa August 13 kwenye uwanja wa taifa lakini pia mchezo huo ulikuwa ni muhimu kwa kocha Salum Mayanga kuelekea msimu mpya wa ligi kuu Tanzania bara ambayo itaanza rasmi August 20.
Wachezaji nyota wa kikosi cha Hans van Pluijm walikosekana kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo majeraha na ugonjwa. Amis Tambwe, Donald Ngoma, Haruna Niyonzima, Kelvin Yondani, Nadir Haroub ‘Cannavaro, Deogratius Munishi ‘Dida’, Juma Abdul, Simon Msuva ni baadhi ya wachezaji walioukosa mchezo huo.