Tume ya Haki na Utawala Bora imeandaa kikao cha pamoja kati ya Chadema, CCM, Jeshi la Polisi na taasisi nyingine tatu, wakati joto la Operesheni Ukuta likizidi kupanda kwa viongozi wa Serikali na vyama vya siasa kutoa kauli zinazotofautiana.
Chadema imetangaza kufanya mikutano nchi nzima kuanzia Septemba Mosi katika operesheni iliyobatizwa jina la Umoja wa Kupinga Udikteta Tanzania (Ukuta), ikidai Serikali ya Awamu ya Tano inakandamiza haki na demokrasia nchini.Kabla ya kikao hicho, viongozi wa upinzni wamekuwa wakisisitiza umuhimu wa kuwapo maridhiano katika suala hilo pamoja na Ukawa kususia vikao vya Bunge vinavyoongozwa na Naibu Spika, Dk Tulia Ackson, lakini kumekuwa hakuna harakati zozote zaidi ya majibizano.
Hali hiyo ilizidi baada ya Chadema kutangaza operesheni hiyo ambayo imesababisha viongozi wa Serikali, hasa wakuu wa mikoa kuanza kutoa matamko ya kupiga marufuku mikutano yote ya Ukuta kwenye maeneo yao huku chama hicho kikisisitiza kuwa kitaendesha operesheni yake bila ya kujali amri ya kuizuia kwa kuwa kina haki kikatiba.