SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatatu, 15 Agosti 2016

T media news

Rais Mbabe au Viongozi wa Dini Waoga?

TAIFA linahitaji uponyaji, maombezi na maonyo kutoka kwa viongozi wa dini zote, anaandika Mwandishi Wetu.

Huduma hizo zinahitajika mno sasa kuliko wakati mwingine, kwa kuwa zipo dalili kwamba Tanzania sasa inaelekea kuwa dola la kipolisi linaloendeshwa kwa mkono wa chuma wa mtu mmoja.

Kwa muda mrefu, viongozi wa dini wamekuwa na heshima ya kusikilizwa na watawala na watawaliwa. Viongozi wa dini wanabeba ujumbe ambao waumini wao wanauchukulia kuwa unatoka kwa Mungu.

Viongozi wa dini ni wawakilishi wa Mungu katika maeneo yao; na kama kauli zao ni adilifu, ni kauli za Mungu. Viongozi wa dini ni jicho la Mungu duniani, ni watetezi wa wanyonge, na walinzi wa wanaoonewa.

Kwa kuwa binadamu ana hulka ya kukimbilia kwa Mungu mambo yanapokuwa magumu, hata jamii inakimbilia kwa viongozi wa dini wakati wa shida.

Bahati mbaya, baadhi ya viongozi wetu wa dini wamekuwa na ukaribu na watawala, unaowafanya wasiweze kuona kasoro za watawala hao. Wamejisahu na kudhani nao ni sehemu ya utawala wa nchi.
Matokeo hawaoni shida za wananchi wa kawaida, hawaoni mateso yanayowakuta; na wakati mwingine wanatumiwa na watawala kunyamazisha wananchi, ili kulinda maslahi ya kisiasa ya watawala.

Sasa nchi imeingizwa katika majaribu. Rais anavunja katiba kwa kutoa matamko na amri dhidi ya wananchi na viongozi wa upinzani. Kuna mtikisiko wa kijamii na kisiasa. Kuna dalili za wazi kwamba udikteta unanyemelea nchi hii.

Ni jukumu la viongozi wa dini kusaidia nchi iondokane na majaribu haya, si kwa kukaa upande wa wenye mabavu, bali kwa kusimama pamoja na wanaonyanyaswa na kukemea au kushauri watawala, ili amani inayoelekea kutoweka irejee.

Watumie fursa hii kuokoa Tanzania, siyo kwa maombi tu, bali vitendo, hatua na kauli za kutetea wanyonge. Wasipofanya hivyo, watakuwa wamepoteza fursa adhimu ya kuinua utukufu wa Mungu mbele ya nguvu za giza.

Na kama wataacha ibilisi akashinda vita hii kwa sababu tu ya hila, njaa, woga, au upendeleo, watakuwa wamepoteza uongozi wao, hata kama watabaki wamevaa majoho; na siku moja wataitwa kutoa ushahidi juu ya madhila yatakayotokea kwa sababu ya ukimya wao.

Chanzo:Mwanahalisionline