RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein, ametoa taarifa rasmi ya Serikali kuhusu kifo cha Rais Mstaafu wa Zanzibar wa Awamu ya Pili, Mheshimiwa Alhaj Aboud Jumbe Mwinyi.
Katika taarifa hiyo aliyoitoa jana kupitia vyombo vya habari, Alhaj Dk. Shein kwa masikitiko makubwa aliwaarifu wananchi kuwa jana tarehe 14 Agosti 2016, Mzee Alhaj Aboud Jumbe Mwinyi amefariki dunia, msiba ambao umetokea nyumbani kwake Mji Mwema, Dar es Salaam.
Alhaj Dk. Shein alieleza kuwa Marehemu Mzee Aboud Jumbe ni Rais Mstaafu wa Zanzibar wa Awamu ya Pili, ambaye vile vile alikuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambapo Marehemu Mzee Aboud Jumbe amefariki dunia baada ya kuugua kwa muda mrefu kutokana na umri wake.
Kwa taarifa ya Alhaj Dk. Shein, maziko ya marehemu yatafanyika leo tarehe 15 Agosti 2016 saa 7.00 mchana ambapo maiti yake itasaliwa katika Masjid Mshawar, Mwembeshauri na kuzikwa nyumbani kwake Migombani.
Aidha, Alhaj Dk. Shein alieleza kuwa kufuatia mchango na juhudi kubwa ambazo Marehemu Mheshimiwa Aboud Jumbe Mwinyi alizichukua katika uhai wake kwa kuitumikia, kuiongoza na kuijenga Zanzibar pamoja na nafasi yake katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Nchi yetu imekabiliwa na msiba mkubwa kwa kifo cha kiongozi huyu mahiri”alieleza Alhaj Dk. Shein katika taarifa hiyo.
Kutokana na msiba huo mkubwa Alhaj Dk. Shein alitangaza rasmi siku saba za maombolezo, kuanzia leo tarehe 15 Agosti 2016 ambapo katika kipindi hicho chote bendera zote zitapepea nusu mlingoti.
Pamoja na hayo, Alhaj Dk. Shein alieleza kuwa utaratibu wa maziko utafuata wasia ambao mwenyewe marehemu aliutoa wakati wa uhai wake.
“Tunaungana na Wanafamilia wote katika kipindi hiki kigumu cha msiba. Naomba kutumia nafasi hii kutoa mkono wa pole kwa wafiwa wote. Tunamuomba Mwenyezi Mungu amjaalie kauli thabit marehemu mzee wetu na amlaze pahala pema peponi, Amin. Inalillahi wainnailaihi rajiun” Alieleza Alhaj Dk. Shein katika Taarifa hiyo.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk