SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumatatu, 15 Agosti 2016

T media news

CUF yampiga chini rasmi Profesa Lipumba


ALIYEKUA Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, ametoswa rasmi kuwania nafasi hiyo katika uchaguzi wa chama hicho unaotarajiwa kufanyika Agosti 21 mwaka huu, kupitia Mkutano Mkuu Maalumu.

Hali hiyo imebainika baada ya kuteuliwa kwa majina ya watu tisa kwa ajili ya kuwania nafasi hiyo ya uenyekiti, huku jina la Profesa Lipumba likikosekana katika orodha hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Mipango na Uchaguzi wa chama hicho, Shaweji Mketo, pia majina manne yameteuliwa kuwania nafasi ya Makamu Mwenyekiti likiwamo jina la Dk. Juma Duni Hajji ambaye anatetea nafasi yake.

Mwishoni mwa mwaka jana, Dk. Hajji  alijiuzulu nafasi hiyo na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambapo aliteuliwa kuwa mgombea mwenza wa urais akiwa na Edward Lowassa aliyeungwa mkono na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi ( Ukawa).

Katika taarifa hiyo, Mketo alisema nafasi nyingine zinazowaniwa kwenye uchaguzi huo ni pamoja na nafasi nne za wajumbe wa Baraza Kuu la Uongozi la Taifa  wa Kanda ya Nyanda za juu Kusini ambapo mjumbe yeyote anaweza kugombea kutoka kanda hiyo na nafasi moja ya mjumbe kutoka Kanda ya Kati ambapo mjumbe yeyote wa Mkutano Mkuu Taifa kutoka kanda hiyo anaweza kugombea.

Alisema nafasi moja ya mjumbe kutoka Kanda ya Ziwa ambayo ni ya mwanamke anaweza kugombea mjumbe yoyote na nafasi moja kutoka Kanda ya Kaskazini ambapo  mjumbe yeyote kutoka kanda hiyo pia anaweza kugombea.

Aliyataja majina tisa ya wanaowania nafasi ya mwenyekiti na taaluma zao kwenye mabano kuwa ni pamoja na Abdul Omary Zowo (Mhandisi wa Ndege za Kivita), James Mahangi (Maabara), Joseph Rhobi (Fundi Seremala), Juma Nkumbi (Mtaalamu wa Kompyuta), Salum Barwany (Fundi Magari), Selemani Khatibu, Twaha Taslima (Mwanasheria), Zuberi Kuchauka (FTC Mechanical) na Riziki Mngwali (Usuluhishi wa migogoro).

Mketo alisema, majina manne ambayo yanawania nafasi ya makamu mwenyekiti na taaluma zao kwenye mabano ni pamoja na Dk. Juma Ameir Muchi (Daktari), Juma Duni Hajji (Mchumi), Mussa Hajji Kombo na Salim Abdallah Bimani.

Alisema, Mkutano Mkuu Maalumu wa kupitisha majina hayo unatarajiwa kufanyika Agosti 21 mwaka huu, jijini Dar es Salaam ambao utaweza kuziba nafasi zilizoachwa wazi

Alisema kuwa chama hicho kilitoa utaratibu wa uchukuaji wa fomu hizo za kuomba nafasi za uongozi ambapo wagombea walitakiwa kwenda kwenye ofisi za  makatibu wa wilaya kwa ajili ya kuchukua fomu hizo, hali iliyosaidia kufanikisha zoezi hilo.

Alisema kutokana na hali hiyo, siku ya mwisho ya kuwasilisha taarifa za wagombea hao kwenye ofisi za makatibu wa wilaya ilikua Agosti  10 mwaka huu.

“Naomba niwashukuru wanachama na viongozi wetu katika ngazi zote nchini kwa kuhamasisha wanachama wenzao ambao wameweza kuchukua fomu za kuwania nafasi ya uongozi ndani ya chama.