Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani limefuta mkutano wa hadhara wa Chadema uliopangwa kufanyika katika Uwanja wa Miembe Saba mjini Chalinze.
Mkutano huo uliokuwa ufanyike jana, ulikuwa uhutubiwe na Waziri Mkuu mstaafu na mjumbe wa kamati ya Chadema, Frederick Sumaye.
Mwenyekiti wa Chadema, Mkoa wa Pwani Baraka Mwago alisema jana kuwa alishangazwa na hatua hiyo ya ghafla ya polisi kwa kuwa mkutano huo ulifuata taratibu zote na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Chalinze, aliruhusu kufanyika kuanzia saa 6.00 mchana hadi saa 12.00 jioni.
Alisema wakati maandalizi yote yakiwa tayari, ilipotimia saa nane mchana waliitwa polisi na kuelezwa kuwa mkutano huo umezuia kwa maelezo kuwa intelijensia ya polisi imeonyesha kuwa ungehudhuriwa na viongozi wengi wa kitaifa, hivyo polisi Chalinze haijajipanga kutoa ulinzi kwa viongozi hao.
“Hii sababu imetushangaza kwa sababu kiongozi wa kitaifa ambaye angehudhuria ni Sumaye peke yake."
Kwa mujibu wa Katiba ya Chadema kipengele cha 7.5.3 (f) inamtambua mjumbe wa kamati kuu au baraza kuu anayeishi katika mkoa kuwa ni mjumbe wa baraza la mkoa husika.
“Kutokana na kipengele hicho, Sumaye ana sifa za kuhudhuria mkutano huu kwa sababu anaishi Kiluvya wilayani Kisarawe,” alisema Mwagu.
Alisema lengo la mkutano huo, lilikuwa ni kuutambulisha uongozi mpya wa Chadema kwa wananchi baada ya kufanyika uchaguzi mdogo Juni 4, mwaka huu wilayani Mkuranga.
Katibu wa Chadema mkoani humo, Halfani Milambo alisema waliandika barua kuwataarifu polisi na likakubali, lakini walishangazwa kuzuiwa baada ya kufika katika Uwanja wa Miembe Saba walikotakiwa kufanya mkutano.
“Tuliwaandikia barua tarehe Agosti 4 na siku iliyofuata Agosti 5 tulikubaliwa na Mkuu wa Polisi Chalinze (OCD), SSP J. Magomi kufanya mkutano kwa masharti,” alisema.
Alitaja masharti ambayo jeshi hilo liliwapa kuwa ni pamoja na kutokuwapo kwa maandamano ya bodaboda, ya miguu au magari, kutokukashifu chama au utawala wa kiongozi yeyote na kuzingatia muda wa kuanza na kumaliza mkutano.
Alisema kuwa cha kushangaza jana baada ya kukamilisha maandalizi yote ikiwamo kufanya matangazo na kufunga vyombo vya muziki, baadhi ya viongozi waliitwa kwenye Ofisi ya Polisi Wilaya ya Chalinze na kuambiwa wasifanye mkutano huo.
Alisema walielezwa kuwa ujumbe ambao unaenea kwenye mtandao unasema mkutano huo utaleta watu wengi sana, hivyo usalama utakuwa mdogo.
Kamanda wa Polisi mkoani Pwani, Boniventura Mushongi alisema lengo la Polisi si kuwakataza kufanya mkutano, lakini kilichoonekana ni kuwa walikiuka maelekezo kwani awali walipaswa kufanya mkutano wa ndani na si wa nje.
“Sisi hatuwakatazi kufanya mikutano yao, lakini ni vema wafuate makubaliano, maana sisi Jeshi la Polisi tuliwaruhusu wafanye mkutano wa ndani lakini tulishangazwa kuona wanaanza kufanya nje huku wakipiga muziki,” alisema.
Mushongi alisema pia polisi inazuia mikutano yote ambayo haina madiwani wala wabunge katika eneo husika, jambo ambalo halikuwa kwenye maelekezo ya OCD.
“Chadema katika eneo la Chalinze hawana diwani wala mbunge, hivyo wamekosa sifa za kufanya mkutano huu. Kama ni kikao cha ndani hatuna tatizo wafanye hata wakialika watu 200,”alisema Mushongi.
Hata hivyo, Mushongi alisema Chadema Pwani walipopeleka barua ya maombi mkutano huo walipewa masharti hayo.
Mbowe: Tuko tayari kwa lolote
Wakati hayo yakiendelea, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe amesema yeye na makamanda wake wako tayari kwa lolote kwa ajili ya kutetea misingi thabiti ya utawala bora unaoheshimu utawala wa sheria.
Akizungumza jana, Mbowe alisema hakuna mtu wa kuwafundisha makamanda wa Chadema, hivyo mikutano ya Ukuta itafanyika nchi nzima kuanzia Septemba Mosi.
“Ambao hawako tayari warudi nyuma, hakuna aliyelazimishwa, watuache sisi tutangulie wa kufa wafe na wa kupona wapone. Haiwezekani mtu apuuze sheria, avunje katiba halafu taifa linyamaze,” alisema.
“Sisi tumeamua kuchukua mzigo huo kwa niaba ya wananchi wote. Kama ataua wacha aue tu, kama atatufunga wacha atufunge tu lakini tutakuwa tumeacha legacy (kumbukumbu) duniani,” alisisitiza.
Mbowe alisema sifa ya kiongozi bora anayeheshimu misingi ya kidemokrasia ni kuheshimu utawala bora unaoheshimu utawala wa sheria.
Kwa mujibu wa Mbowe, Rais anakiuka Katiba na sheria za nchi zinazoruhusu vyama vya siasa kuendesha mikutano ya hadhara na hakuna mtu ndani ya CCM anayezungumzia hilo.
Mbowe alisema Rais amejisahau kuwa yeye (Mbowe) ni mwenyekiti wa taifa kama alivyo Rais, hivyo anastahili kuzunguka nchi nzima kujenga uhai wa chama.
“Rais anazunguka kwenye mikoa anavisema vyama vya upinzani na kutoa amri mbalimbali lakini sisi (upinzani) hatuna jukwaa la kujibu au kutoa ufafanuzi. Anasema tusubiri hadi 2020,”alilalamika Mbowe.
“Rais anatoa amri, wakuu wake wa mikoa wanatoa amri, wakuu wa wilaya wanatoa amri, watu wanafukuzwa kazi ovyo. Nchi haiwezi kwenda kwa staili hii,” alisema.
“Wewe unanyanyuka tu na kusema watu wahamie Dodoma kivipi? Issue ya kuhamia Dodoma ni suala la kitaifa siyo mamlaka ya mtu mmoja tu kwa kuwa ni Rais.”
“Hata Nyerere 1973 alipopitisha hoja ya watu kuhamia Dodoma kilikuwa ni kikao cha NEC ya Tanu. Mpaka leo hakuna sheria ya kuhamia Dodoma na nchi hii inaoongozwa kwa sheria.”
Mbowe alisema kwa kutambua kuwa hakuna sheria ya kuhamia Dodoma, ndiyo maana Ilani ya CCM (2015-2020) imeeleza kutengeneza sheria ya kuhamia makao makuu Dodoma.
“Hakuna sheria. Rais hawezi kuamua matakwa yake binafsi yakawa ni sheria ya nchi. Alipaswa apeleke muswada wa sheria bungeni na ipitishwe na Bunge siyo kauli ya mtu mmoja,” alisisitiza Mbowe.
Lissu: Tutafuata sheria
Wakati huohuo, mwanasheria Mkuu wa Chadema na mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu amesema katika utekelezaji wa Ukuta watafuata sheria kwa kupeleka barua za taarifa ya mikutano kwa wakuu wa polisi nchi nzima saa 48, kabla ya kuanza mikutano hiyo Septemba Mosi mwaka huu.
Akizungumza juzi katika mahojiano na Redio ya Sauti ya Ujerumani (DW), Lissu alisema mikutano hiyo itafanywa kwa kufuata sheria na taratibu ikiwamo kutoa taarifa kwa wakuu wa polisi wa wilaya.
Lissu ambaye aliachiwa na mahakama juzi kwa dhamana, alitoa kauli hiyo baada ya kuulizwa kwanini chama chake kisitafute njia mbadala ya operesheni Ukuta ambayo Serikali imesema itakabiliana nayo kwa njia yoyote ile.
“Tumesema hatutafanya mkutano wowote usiokuwa na taarifa.Tutapeleka taarifa kwa wakuu wa polisi wilaya wote Tanzania nzima kama inavyotakiwa. Sasa hiyo hatuvunji sheria, tunatekeleza sheria,” alisema Lissu.
Mbunge huyo, ambaye anakabiliwa na mashtaka ya uchochezi na kuidharau mahakama, alibainisha kuwa mikutano ya hadhara kuanzia Septemba Mosi, itafanyika kwa mujibu wa sheria za nchi kama Katiba ya nchi na sheria ya vyama vya siasa inavyoeleza.
Alisema sheria inasema chama cha siasa ambacho kimeandikishwa kikitaka kufanya mkutano wowote wa hadhara wa siasa, kinatakiwa kupeleka barua ya taarifa kwa mkuu wa polisi wa wilaya saa 48 kabla ya mkutano huo.
“Sheria inasema huyo ambaye tunampelekea taarifa atupe ulinzi kwenye mikutano yetu. Ndicho tunachotaka,”alisema Lissu.
Alipoulizwa kama ni sawa iwapo polisi ikisema haiwezi kuwapa ulinzi na wasifanye mkutano katika eneo husika kwa wakati huo, Lissu alijibu, “(OCD) Ana uwezo wa kutuambia msifanye leo, msifanye kwenye eneo hili au msifanye saa hii, lakini hana uwezo wa kukataa katakata.”
Mbunge huyo alisema kilichotokea nchini na kinachofanyika sasa si mikutano kudhibitiwa bali inakatazwa.
“Hakuna sheria inayokataza au inayowapa mamlaka ya kukataza mikutano moja kwa moja kama hakuna tangazo la hali ya hatari,” alisema Lissu.
Alisema kama Magufuli hataki mikutano atangazie dunia kwamba Tanzania ina hali ya hatari.
“Akitangaza hali ya hatari tutamwelewa na wengine tutamuuliza kilichotokea ni kitu gani mpaka kuwe na hali ya hatari,”alisema Lissu.