Mchezaji mmoja wa kuogelea, judo mchezaji mmoja, pamona na riadha wachezaji wawili, hawa ni wachezaji wa kitanzania walioshiriki michuano ya Olympic 2016 inayoendelea Rio, Brazil.
Nimekutana na wadau wa mchezo wa Judo na hapa tunapiga stori, wakwanza kabisa ni Zaid Hamisi ambaye ni kocha mkuu wa timu ya taifa ya Tanzania ya mchezo wa judo ambaye alikuwa ameambatana na mchezaji wake Andrew Thomas.
Naanza kufanya mahojiano na mchezji Andrew Thomas kisha baadae naendelea na kocha wake.
shaffihdauda.co.tz: Watanzania walitarajia medali kutoka kwako lakini umetoka mikono mitupu, tatizo lilikuwa nini?
Andrew Thomas: Kwenye mashindano kuna kushinda na kushindwa, kwahiyo ni sehemu ya mashindano vilevile.
shaffihdauda.co.tz: Hii ni mara yako ya ngapi unashiriki mashindano makubwa kama ya Olympic?
Andrew Thomas: Ni mara yangu ya kwanza kushiriki mashindano ya Olympic.
shaffihdauda.co.tz: Huu mchezo ulianza lini kujifunza?
Andrew Thomas: Tangu nimeanza kucheza judo mpaka sasa nina miaka kama 11 hivi.
shaffihdauda.co.tz: Ulishawahi kushiriki mashindano mengine zaidi ya haya?
Andrew Thomas: Ndiyo nimewahi, nimeshiriki Common Wealth games na All Africa games.
shaffihdauda.co.tz: Matarajio yako kabla ya mashindano yalikuwaje?
Andrew Thomas: Kila mtu anaposhiriki mashindano anatarajia kufanya vizuri, kwahiyo mimi pia kutokana na kiwango nilichokuwanacho nilikuwa natarajia kufanya vizuri, lakini ndiyo hivyo matokeo yamekuwa sivyo ambavyo nilikuwa natarajia.
shaffihdauda.co.tz: Nini kilikukwamisha?
Andrew Thomas: Nilizidiwa mbinu ya chini, unajua judo unaweza ukashinda chini, unaweza ukashinda juu lakini unaweza ukashindwa vilevile kwa mbinu za chini kwahiyo nilizuiliwa chini nikashindwa kutoka basi mpinzani wangu akashinda.
shaffihdauda.co.tz: Mpinzani wako alikuwa anatoka taifa gani?
Andrew Thomas: Nilicheza na mu-australia.
shaffihdauda.co.tz: Kwa upande wako kocha, unazungumziaje kiwango cha kijana wako alichokionesha kwenye mashindano?
Andrew Thomas: Naweza kusema ame-improve kwasababu nafasi ya kuja huku aliipata kutokana na kiwango alichokionesha katika mashindano ya Afrika. Wanaoshiriki Olympic upande wa judo wanakuwa ni mabingwa wa mabara, kwahiyo kuna vigezo vyake. Ili uchaguliwe kuja kushiriki Olympic upande wa judo lazima ufikishe pointi 600, pointi hizo zinapatikana vipi, ukishiriki mashindano ya dunia mshindi wa kwanza ndiyo anakuwa amefikisha pointi 600 mashindano ya Afrika mtu wa kwanza pia anakuwa amepata pointi 600.
Sisi tulishiriki mashindano ya Afrika lakini yeye hakuweza kupata pointi 600 lakini pointi zake na kiwango chake waliona anao uwezo wa kushiriki mashindano haya kwahiyo alipata nafasi maalumu kwasababu umri wake ni mdogo na kiwango chake ni kizuri, kwahiyo akapewa hii nafasi ya World card kuja kushiriki mashindano haya ya Olympic.
shaffihdauda.co.tz: Kipi kimekufanya uvutiwe na kiwango cha mchezaji wako licha ya kushindwa kutwaa medali?
Kiwango chake nimekipenda kwasababu ni mara yake ya kwanza kushiriki mashindano kama haya na kile nilichomwambia akafanye nimeona amefanya.
shaffihdauda.co.tz: Kocha unawaambia nini vijana wa Tanzania ili na wenyewe waweze kupata fursa kama hii ya kushiriki mashindano makubwa kama haya ya Olympic.
Kikubwa ni kwamba, watu wanatakiwa wafanye mazoezi, tunaona wenzetu wanapata medali sio kama wamelala na kuamka, wanajipanga. Hii Olympic ikiisha miaka minne mingine ijayo wanajua nini wafanye ili mtu anapoenda Tokyo 2020. Wanamipango na wanapata ushirikiano kutoka kwa serikali zao.
Tanzania tunawatu wanaweza judo, wapo watu wenye vipaji na umri wao bado unaruhusu, wanaweza kufikia level kubwa pamoja na haya mashindano ya Olympic sio ya kujiandaa kwa miezi miwili au miezi mitatu.
Kunatakiwa kuwe na program za muda mrefu ambazo zinahusisha kambi za nje ya nchi. Hawa tunaoona wanafanikiwa wanaweka kambi za nje ya mataifa yao kwahiyo wachezaji lazima wapate mazoezi makali kwenye nchi ambazo michezo hiyo ipo juu.
Tunakosa ushirikiano kutoka serikalini, serikali haiwezi kujitoa kwenye mambo kama haya. Nchi zote ambazo zimekuja hapa fatilia utaambiwa, taifa kama Georgia wamewekeza dola za Marekani milioni 60 katika maandalizi ya miaka minne hii na wameshapata medali mbili za dhahabu. Nchi kama Australia wamewekeza milioni 40 katika uogeleaji na wamepata medali tatu, lakini sisi mpaka huyu mchezaji ameweza kufika hapa ni jitihada zake binafsi pamoja na mimi kama kocha na mlezi wake.
Sisi tunakomaa wenyewe tunahangaika na maandalizi lakini ukiuliza Tanzania kama kuna centre kwa ajili ya maandalizi ya Olympic hatuna ya mchezo wowote.
Kwanza Tanzania kama wanataka mafanikio lazima tuwe na centre yetu ya maandalizi ya Olympic ya michezo yote kitaifa ili tukishachagua wachezaji kwenye kila mchezo tunawapeleka huko tunawaweka wanafanya mazoezi.
Wizara husika inabidi itusikilize sisi watalam ambao tumetoka tumekuja huku tumeona wenzetu wanafanya nini. Hakuna nchi hata moja kutoka Afrika ambayo imepata medali kwenye mchezo wa judo.
Kama nchi lazima tuwe na sera ya taifa ya michezo, itatusaidia sisi watu wa ufundi ili kutengeneza wanamichezo kufikia katika kiwango fulani. Tulivyotoka Jumuia ya Madola tulifanya kikao na nilitoa mawazo jinsi gani nchi za wenzetu wanavyojali maslahi ya wachezaji.
Sisi Tanzania tunatatizo katika hilo kwasababu linatokea mara zote lakini tulitegemea mwaka huu haiwezi kuwa hivyo ila muelekeo unavyokwenda yunaona itakuwa hivyo kwasababu hata timu wakati inaagwa na Naibu Waziri, aliongea mbele ya waandishi wa habari kwamba kila kitu kipo tayari wachezaji watapata stahiki zao wataenda kwenye mashindano lakini tumefika huku wakati watu wanataka kuondoka tumepewa dola kama 500 kwa ahadi kwamba tukirudi pesa nyingine tutamaliziwa.
Wakati tupo kwenye michezo tukasomewa na chief wetu kwamba ametumiwa ujumbe kutoka Wizarani kwamba lile fungu walilotegemea kuwapa wanamichezo, halitakuwa kama vile walivyoahidi kwahiyo hata hicho kidogo ambacho waliambiwa watapewa, hakipo watapewa kidogo hawa wachezaji wanaumia.
Mchezaji anapokuja Olypic ni sehemu ya kubadilisha maisha yake kimichezo, kiakili hata kiuchumi akirudi hata wale wenzake ambao hawakufuzu wanaona kunatofauti ili nao wawe na moyo wa kupambana kufuzu kwa ajili ya mashindano yanayofuata na kupata medali.