Jeshi la Yemen limefanikiwa kuangamiza makumi ya mamluki wa Saudi Arabia mashariki mwa mji mkuu Sanaa.
Duru za kijeshi zimearifu kuwa, mamluki hao walianzisha makabiliano dhidi ya jeshi la Yemen kwa lengo la kudhibiti wilaya ya Nihm, mashariki mwa Sanaa, kaskazini mwa nchi hiyo ya Kiarabu.
Askari vamizi wa Saudia nchini Yemen
Hata hivyo askari wa Yemen kwa ushirikiano na vikosi vya kujitolea vimewakabili mamluki hao wa Aal-Saud na kuangamiza 52 miongoni mwao. Shirika la habari la Saba limeripoti kuwa, baada ya kushadidi makabiliano hayo, mamluki hao wa Saudia walilikimbia eneo hilo na kuacha wenzao 17 nyuma wakiwa na majeraha ya risasi.
Wanajeshi wa Yemen
Huku hayo yakijiri, raia wanne wamejeruhiwa katika hujuma ya anga ya ndege za utawala wa Riyadh katika mji wa Shaqra katika mkoa wa Abyan, kusini mwa nchi. Aidha ndege hizo zimeshambulia wilaya ya al-Maton katika mkoa wa kaskazini wa al-Jawf
Athari za mashambulizi ya anga ya Saudia nchini Yemen
Maelfu ya raia wa Yemen wameuawa na kujeruhiwa katika mashambulio hayo na taasisi nyingi za miundombinu ya nchi hiyo masikini zimeteketezwa bila ya watawala wa Aal Saudi kufikia malengo yao yasiyo ya kibinadamu tokea Machi mwaka jana.