NA JOSEPH SHALUWA
Ni mrefu, mwenye ngozi yenye rangi ya dhahabu. Ana macho meupe, pua fupi, midomo minene iliyofunika meno yaliyopangika vyema kinywani na kutengeneza mwanya mdogo wa kichokozi katikati.Sauti yake nyembamba ni kivutio kingine, shingo ndefu kama ya twiga ni kati ya sifa zinazomuacha kwenye orodha ya warembo wa Tanzania wenye mvuto kwa mwaka wa kumi sasa.
Usisahau kwamba mwaka 2013 alishinda Tuzo ya Msichana Mwenye Mvuto Zaidi (Sexiest Girl Award) ya gazeti moja la wiki nchini akiwamwaga washiriki wenzake waliongia fainali, Elizabeth Michael ‘Lulu’, Nelly Kamwelu, Jacqueline Wolper na Jokate Mwegelo.
Wema Isaac Sepetu ni kati ya warembo wachache nchini kutokea Miss Tanzania wenye kismati cha aina yake. Wamepita warembo wengi sana tangu yalipoanzishwa mashindano hayo mwaka 1994, lakini wengi wameshapotea kwenye ramani.
Achana na walioshinda nyuma yake, tangu aliposhinda Wema mwaka 2006, warembo wengine takribani wanane waliomfuata, wengi wamesahaulika kabisa. Nitakukumbusha mwishoni.
Ni rahisi kusema mwaka 2006 ulikuwa mwaka wa bahati kwa washiriki na hasa wale walioshinda nafasi za juu. Kati ya warembo watano waliongia Tano Bora, wanne mpaka sasa wanaendelea kutesa kwenye sanaa mbalimbali.
Nyuma ya Wema kuna Jokate Mwegelo ambaye ni modo, mwigizaji na mwanamuziki wa Bongo Fleva, Lisa Jensen – mwanamitindo na mwigizaji na Irene Uwoya aliyechukua namba 5 akitesa kwenye filamu za Kibongo.
Pamoja na kwamba warembo wote wanne kutokea Miss Tanzania 2006 wapo kwenye game, Wema anaonekana kukubalika zaidi na mashabiki. Hiyo ni nyota ya ajabu kwa mlimbwende huyu.
Kwa lugha nyepesi, naweza nikasema Wema ni brand – bidhaa. Ni taasisi kubwa ambayo inaweza kutengeneza fedha nyingi. Wema ni utajiri. Kupitia kipaji chake, anaweza kupata fedha nyingi mbali na umaarufu ambao pengine unamsaidia mambo mengi.
Nimesukumwa kuandika makala haya ili kumuibua usingizini na kama alikuwa analitambua hili, basi ajue kuwa wapo wanaliona hilo kwa jicho pana, hivyo ingekuwa bora na faida kwake kama akianza haraka mapema ili kutengeneza umilionea.
MVUTO WA WEMA
Kama unabisha kuwa Wema siyo brand, hakubaliki na hana kismati, fanya uchunguzi mwepesi ambao utakupa majibu ya haraka. Andika chochote kuhusu Wema mtandaoni ukimsema vibaya, uone kazi ya mashabiki!
Wema hana sababu ya kujibu chochote. Hata ukimchafua kwa staili gani, wapo mashabiki zake huko, watasimama kwa ajili yake. Wema anapendwa, anakubalika.
Kingine kinachomsaidia kukubalika na kupendwa ni namna anavyoguswa na mambo mbalimbali ya kijamii. Amewasaidia wengi wakiwemo mastaa. Kajala Masanja ni miongoni mwao.
Wakati akiwa kwenye sakata la kwenda jela au alipe faini, ni Wema ndiye aliyotoa Shilingi milioni 13 kumsaidia kurejea uraiani na kupishana na mateso ya nyuma ya nondo. Wema hachafuki!
NINI KIMEMPATA WEMA?
Wakati anaanza alijitahidi kuonyesha nia ya kusaka mafanikio, lakini kwa sasa spidi yake imepungua. Wema alikuwa na kasi ya kucheza sinema. Alikuwa miongoni mwa wasanii wa kike wanaolipwa ghali zaidi.
Katika kundi hilo walikuwemo Aunt Ezekiel, Rose Ndauka, Irene Uwoya, Jacqueline Wolper na Shamsa Ford. Mwaka 2013, Wema alifungua kampuni yake ya utayarishaji filamu, Endeless Fame Films.
Lilikuwa wazo zuri la kibiashara.
Lakini wazo hilo hakulitendea haki, kwani mwaka mmoja baadaye alifunga ofisi hiyo. Nini kimetokea? Wema anapaswa kujitazama upya na kuangalia namna ya kusimama tena. Mtaji bado anao - ni jina lake tu.
MANAGEMENT ZAIDI
Wema anaweza kutengeneza fedha zaidi kama akiwa na uongozi imara zaidi. Haina maana kwamba, Martin Kadinda siyo meneja mzuri, la hasha! Kadinda ni kijana mjanja, mchakarikaji na mbunifu.
Ndiye aliyeharakisha na kushughulikia wazo la bidhaa ya lipstick yenye jina la Kiss by Wema Sepetu. Duka linalouza bidhaa hizo lipo Mwenge jijini Dar es Salaam. Hongera sana Kadinda.
Lakini tukiangalia mafanikio ya mastaa wengi, si ya kutegemea meneja mmoja. Unaweza kuwa na mmoja anayesimamia jumla, lakini wengine wawili au watatu wakawa wa kubuni idea zaidi za biashara na kutoa ushauri.
Sipati picha, ikiwa watu kama Ruge Mutahaba, Said Fella au Babu Tale wangekuwa kwenye crew ya management ya Wema ingekuwaje! Naamini tungekuwa tunamwongelea Wema mwingine.
Si dhambi kuwa na meneja zaidi ya mmoja. Mwangalie Diamond anavyotusua kimafanikio, ni kwa sababu amezungukwa na mameneja wanaoshindana kuumiza vichwa kubuni mawazo ya biashara ya kumpaisha zaidi na zaidi.
Hata Wema pia anaweza kutumia mbinu hiyo ili kutumia jina lake kujiweka pazuri kimafanikio. Kama kuna mtu amepata kumwambia kuwa eti jina lake limeanza kuchuja, anamdaganya sana. Muda bado unao Wema. Ni wewe tu.