WAZIRI wa mambo ya ndani ya nchi Mwigulu Nchemba, amesema kuwa Serikali itahakikisha inakabiliana kwa nguvu zote na tatizo la makazi ya askari polisi nchini ili kulipa hadhi jeshi hilo ambalo linakabiliwa na changamoto mbalimbali.
Nchemba aliyasema hayo jana wakati alipokuwa akizungumza na maafisa wa jeshi hilo pamoja na askari wa kawaida wa mkoa wa Dodoma katika kikao kazi kilichofanyika kwenye bwalo la jeshi hilo mjini Dodoma.
Mwigulu alisema kuwa mojawapo ya suala ambalo wizara yake italipa kipaumbele ni makazi ya askari wa jeshi hilo ambayo mengi hivi sasa yamechoka na kukosa hadhi ya kutumiwa na askari wa jeshi hilo.
“Suala la makazi tutalipa kipaumbele kikubwa sana na tutaanza hatua kwa hatua kulifanyia kazi suala hili ili askari wetu waondokana na adha hii wanayoipata kwa muda mrefu sasa,”alisema Mwigulu.
Alisema kero nyingine watakayoifanyia kazi ni kuhakikisha kuwa mazingira ya kufanyia kazi kwa askari polisi yanaboreshwa kuanzia kazini kwao na pia kwenye makazi yao.
“Kumekuwapo na tatizo la mafuta kwa jili ya magari mnayoyatumia … hata tukio likitokea mnashindwa kufika kwa kukosa mafuta.
"Pia kuna maslahi duni, umeme maofisini pamoja na nyumbani mnapoishi imekuwa ni kero kubwa kwenu hivyo sisi kama wizara tutahakikisha haya yote tunayaondoa,” alisema Mwigulu.
Katika hatua nyingine, Mwigulu alitoa rai kwa askari polisi nchini kuhakikisha kuwa wanazingatia miiko ya kazi yao kwa kufanya kazi kwa kuzingatia maadili kama ambavyo walivyofundishwa katika mafunzo yao.
“Mimi uwepo wangu hapa sijaja kuwafundisha kazi kwakuwa tayari kazi yenu mnaijua… ambayo mmefundishwa mkiwa chuoni. Hivyo sisi kama wizara jukumu letu ni kuweka mazingira wezeshi ili mfanye kazi zenu katika mazingira mazuri,” alisema.
Aidha alilitaka jeshi hilo kutumia nguvu katika mahali panastahili tu kufanya hivyo ili hata mwanachi akisikia utendaji wao ajivunie uwapo wa jeshi hilo.
“Tumieni nguvu mahali mbapo Mtanzania wa kawaida akisikia ajivunie uwapo wenu kama ambavyo mmejitahidi katika suala la madawa ya kulevya. Kama tutaweza kuubaini mnyororo huo na kuukata, mwanchi wa kawaida atajivunia,” alisema.
Aidha alisema kuwa jeshi hilo bado lina kazi kubwa ya kufanya ili kukomesha mtandao wa watu wanaojihusisha na madawa ya kulevya nchini na pia akalitaka jeshi hilo kuhakikisha linakuwa mtetezi wa wanyonge.
Kamanda wa polisi mkoa wa Dodoma, Lazaro Mambosasa, awali akimkaribisha Waziri Mwigulu alisema kuwa jeshi hilo limejipanga vilivyo katika kuhakisha uhalifu unakomeshwa mkoani hapa.
“Mweshimiwa waziri mwenye utakuwa ni shahidi ukiwa katika vikao vya bunge uliona namna ambavyo amani na usalama ulikuwepo wa kutosha. Hii yote ni kutokana na kujipanga vizuri kwa jeshi la polisi mkoani hapa,” alisema Mambosasa.