Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, Dkt John Pombe Magufuli amesisitizia kwa mara nyingine tena azma yake ya kuhakikisha kuwa makao makuu ya serikali yanahamia mkoani Dodoma.
Akihutubia kwenye maadhimisho ya Siku ya Mashujaa yaliyofanyika kitaifa mkoani Dodoma Jumatatu hii, Rais Magufuli amesema anashangaa kuona kuwa wabunge wengi huishi mjini humo lakini bado suala la serikali kuhamia huko limekuwa gumu.
“Makao makuu yapo Dodoma, Dodoma ndiyo penyewe, haiwezekani wabunge zaidi ya mia saba wanakaa Dodoma na makao makuu ya chama changu ninachokiongoza yapo Dodoma,” amesema.
“Tukiadhimisha maadhimisho hayo hatuwezi kumsahau Baba wa Taifa letu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na mawazo yake ya makao makuu kuwa Dodoma lazima tuyaheshimu na kutopinga maneno ya mzee huyu,” amesisitiza Rais.
Jumamosi iliyopita wakati wa mkutano mkuu wa Chama cha Mapinduzi, CCM uliofanyika mjini humo, Rais Magufuli aliahidi kuwa hadi anamaliza miaka yake mitano ya awamu yake ya kwanza uongozi, atahakikisha serikali inahamia Dodoma.
Rais Mafuguli pia alitumia fursa hiyo kuwaombea dua kwa mwenyezi Mungu mashujaa walioshiriki kwenye ukombozi wa taifa.
“Wapo mashujaa wetu waliotoa roho zao kwa ajili ya taifa letu wakati wakipambana na ukoloni. Kuna watu waliotoa maisha yao kwaajili ya kutetea maisha yetu, wapo mashujaa wetu waliopotea wakati tulipovamiwa na Nduli Idd Amin. Wapo mashujaa wetu waliofariki katika mapinduzi matakatifu kule Zanzibar, wapo mashujaa wetu walioshiriki katika kukomboa nchi mbalimbali za Afrika ili na zenyewe zipate uhuru, wapo waliofariki Msumbiji, Comoro,Afrika ya kusini na maeneo mengine mengi,” alisema Rais Magufuli.
Aliwashukuru viongozi wote waliohudhuria maadhimisho hayo na pia kuwapongeza viongozi wa dini mbalimbali waliokuwepo na kuwaombea kwa Mungu awabariki kwa kuhudhuria.
Pia alidai kuwa Tanzania ni kisiwa cha amani na kusisitiza amani iliyopo Tanzania isipotee. “Kila mmoja aliopo hapa na tuliopo Tanzania tujiulize tumeikuta amani yetu tuijenge na kuidumisha amani yetu. Nina uhakika Watanzania kwa umoja wetu na mshikamano wetu nina uhakika tutakuwa tumewaenzi vizuri mashujaa wetu waliotangulia mbele ya haki. Tuwaombee mashujaa hawa muhimu kwa taifa letu ili kama kuna mahali popote walifanya dhambi katika matendo yao wakati wa kutetea taifa hili Mungu akawasamehe dhambi na awawezeshe kupumzika kwa amani. Ninajua na sisi siku moja tutawakuta huko.”
BY: EMMY MWAIPOPO