Baada ya Kamati ya Maadili, Haki na Madaraka ya Bunge kuwatia hatiani wabunge saba kwa makosa mbalimbali ikiwemo kudharau madaraka ya bunge ambapo wabunge Easther Bulaya na Tundu Lissu wameadhibiwa kutokuhudhuria vikao vilivyobaki vya mkutano wa tatu na vikao vyote vya mkutano wa nne.
Wabunge Pauline Geku, Halima Mdee, Zitto Kabwe, Godbless Lema wamepewa adhabu ya kutokuhudhuria vikao vyote vilivyobaki vya mkutano wa tatu na Mbunge John Heche hatohudhuria vikao kumi vya mkutano wa tatu. Makosa hayo waliyafanya mkutano wa pili mwezi January.
Baada ya adhabu hiyo kwa wabunge, ACT Wazalendo wametoa tamko lao ambapo wameyazungumza haya……
’Chama cha ACT Wazalendo kimesikitishwa na kitendo cha ugandamizaji wa demokrasia kilichofanywa na wabunge wa CCM kwa kuwasimamisha ubunge wabunge wa upinzani akiwemo kiongozi wa chama chetu Zitto Kabwe’
’Katikati ya masikitiko hayo tunafarijika kuona wabunge hao wameondolewa kwa sababu ya misimamo yao ya kutetea maslahi ya wananchi’
’Tungesikitishwa zaidi kama mashujaa wetu hawa wangeondolewa bungeni kwa sababu ya ulevi au wawe sehemu ya wagonga mihuri ya masuala ya hovyo hovyo yanayosimamiwa na serikali ya chama cha Mapinduzi (CCM)’
’Kwa sababu hiyo ya kusimamia maslahi ya wananchi sisi kwetu ni mashujaa na kwa maana hiyo Chama chetu kinaandaa maandamano makubwa jijini Dar Es Salaam kuwapokea mashujaa wa wananchi’