Kampuni ya kufua umeme ya Symbion imesema maneno ya uzushi na ukiukwaji wa mikataba unaofanywa na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) utaligharimu Taifa na kulitaka shirika hilo kusema ukweli kuhusu makubaliano yao.
Kampuni hiyo pia imeeleza kuwa mwishoni mwa mwaka jana, kigogo mmoja wa Tanesco (ametajwa jina lakini tunalilisitiri jina lake kwa sababu hakupatikana jana) alisaini mkataba na Symbion wa kuliuzia umeme shirika hilo la umma kwa miaka 15.
Taarifa iliyoletwa jana kwa vyombo vya habari na mshauri wa Symbion, Julius Foster inaeleza kuwa taarifa zote zinazotolewa na Tanesco kuhusu uhusiano wao wa kimkataba ni za uongo na zimewashtua kwa kuwa shirika hilo la Serikali halijawahi kuieleza Symbion kuhusu tuhuma hizo.
“Kama itatokea suala hili likaleta mgogoro wa kitaifa, tunataka Tanesco na Serikali na yeyote yule kufafanua masuala haya kwa kiapo na mbele ya mahakimu na tutaujulisha umma kila kitu,” inasema taarifa hiyo.
“Zaidi ya barua ambayo walitaka kusitisha majadiliano na Symbion, hajawahi kujadili na sisi jambo lolote ambalo (kigogo huyo wa Tanesco), analizungumza sasa kwenye vyombo vya habari huko Tanzania.”
Hivi karibuni, iliripotiwa kuwa Tanesco imepanga kufungua kesi ili kusitisha mkataba na Symbion kutokana na wingi wa kesi dhidi ya kampuni hiyo ya Kimarekani.
Miongoni mwa kesi hizo ni ile iliyofunguliwa Mahakama ya Biashara na East African Cables dhidi ya Symbion Tanzania Ltd kutokana na deni la Sh6.372 bilioni. Tanesco ina hisa kwenye kampuni ya East African Cables.
Kadhalika, taarifa hizo zinaeleza kuwa Tanesco imeamua kusitisha mkataba huo kutokana na Symbion kudaiwa Sh6 bilioni na kampuni ya Oilcom, yakiwa ni malimbikizo ya malipo ya usambazaji wa mafuta kwa miaka mitatu.
Hivi karibuni, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo alisema mikataba yote ya Tanesco na kampuni za kufua umeme si mizuri na haina manufaa yoyote kwa Taifa.
Akijibu swali bungeni, Profesa Muhongo alikiri kwamba deni la Tanesco ni kubwa na limesababishwa na uongozi dhaifu, rushwa, wizi na mikataba mibovu ambayo Tanesco imeingia. Alisisitiza kwamba hakuna mkataba unaolinufaisha Taifa.
Taarifa ya Symbion inaeleza kuwa wakati Tanesco inataka kusitisha mkataba huo, imeshindwa kulipa kiasi cha kati ya dola 25 milioni za Marekani na dola 80 milioni katika kipindi cha miaka mitano.
“Pamoja na deni hilo katika kipindi cha miaka mitano, hatukuwahi kuzima umeme, tukaendelea kuzalisha umeme na kujenga vituo vya dharura vya kufua umeme kwa kuwa kama si hivyo, Tanzania ingeingia gizani kwa sababu kiwango cha maji cha Mtera, Kihansi na Kidatu kilikuwa chini,” inasema taarifa hiyo.
“Kwa kuwa sasa mabwawa yamejaa ndiyo mnataka kuvunja mkataba?
“Tukifanya hivyo, wanaoathirika ni Watanzania. Tuna uhakika baadhi ya vigogo wa Tanesco hawaathiriki kwa sababu wana jenereta, ni wananchi ndiyo wanaoathirika.”
Taarifa hiyo inasema pamoja na kauli ambazo imeziita za uzushi zinazotolewa na shirika hilo, bado Symbion inasubiri majibu ya barua ambayo iliituma kwa Serikali wiki tatu zilizopita kuhusu mkataba huo.