SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumapili, 29 Mei 2016

T media news

SIMEONE, KOCHA MWANAHARAKATI NA SHUJAA WA ATLETICO MWENYE NDOTO KALI ZA UEFA


Na Mahmoud Rajab

Diego Simeone ni mpambanaji. Kamwe hilo huwezi kupinga na mara zote yeye kama kocha na wachezaji wake hufanya hivyo kwa maslahi ya timu kutokana na timu kutokuwa na bajeti ya kununua wachezaji kwa pesa nyingi.

Kuna wakati aliwahi kuhojiwa juu ya aina ya uchezaji wake kwamba kwanini uko ‘too physical’? alichokisema ni kwamba: ‘Wazazi wangu waliniambia nicheze mpira kama mwanajeshi”. Diego Simeone ni mtu ambaye anaamini kila mchezaji kwenye timu yake apambane mpaka tone la mwisho. Falsafa yake ni kwamba huwa kama mchezaji hataki kujitoa kwa asilimia zote kwa ajili ya timu, basi hawezi kufanya naye kazi.

“Nawashukuru sana wazazi waliowazaa wachezaji hawa”, hiyo ni kauli ya Simeone aliyoitoa wakati ameshinda game ya Champions League dhidi ya Chelsea mwaka 2014. Ni maneno yaliyolenga kuwapa morali wachezaji wake na hatimaye kutinga fainali na kufungwa na Real Madrid. Matokeo yale yalimuumiza kutokana na kufungwa kusikotarajiwa baada ya kuhimili dakika zote wakiongoza mpaka pale Ramos alipoisawazishia Real na hatimaye kuongezwa muda wa ziada ambapo waliishia kufungwa magoli 4-1.

Ni miaka miwili imepita sasa, Atletico wamefanikiwa kuingia fainali na kukutana tena na Real Madrid. Jana tumeshuhudia wakiwa na utulivu wa aina yake. Wakiwa wameanza kipindi cha kwanza kwa kucheza soka la taratibu, Atletico walijikuta wakiruhusu goli katika dakika za mwanzo tu (dakika ya 15) lililofungwa na Sergio Ramos, goli ambalo hata hivyo linahisiwa kuwa la offside kutokana picha mbalimbali zilizosambaa.

Mpaka kipindi cha kwanza kinamalizika matokeo yalibaki kuwa 1-0. Atletico walikuja kipindi cha pili wakiwa na ari na hamasa ya kusawazisha na pengine kumaliza kabisa mchezo. Alikuwa ni Fernando Torres aliyechezewa madhambi na Pepe na mwamuzi kuamuru ipigwe penati na ndipo Antoine Griezman alipokosa mkwaju huo.

Ikumbukwe tu wikiendi iliyopita Antoine Griezmann alikosa pia penati wakati wakiwa mazoezini, pale kocha wao alipoamuru kikochi cha wachezaji 11 ambacho kilikuwa tayari kucheza na Real fainali kucheza na kikosi kinachoundwa na wachezaji wa akiba ili kuujaribu mfumo wa 4-3-3. Mchezo huo ulimalizika kwa pande zote mbili kutofungana, pengine penati aliyokosa Griezmann jana ilikuwa ni athari ya ile aliyokosa mazoezini, lakini sitaki kuamini hivyo sana kwa sababu makosa ni sehemu ya mchezo.

Hapa ndipo unapoona tofauti ya Simeone na makocha wengine. Baada ya tukio hili Griezmann alikuwa ni kama ametoka nje ya mchezo, lakini Simeone alimwita na kumpa moyo na kumwachia akafanye aliyomwelekeza.

Kilichotokea ni kwamba baada ya muda Atletico waliendelea kufanya mashambulizi langoni mwa Real huku Simeone akiwachagiza mashabiki kuishangilia timu na kuipa morali. Morali ya wachezaji wa Atletico ambayo inachagizwa na kocha wao iliendelea kupamba moto na kusababisha safu ya kiungo na ushambuliaji ya Real iliyokuwa ikiongozwa na Karim Benzema, Cristiano Ronaldo na Gareth Bale kutooneakana.

Kutokana na presha kubwa ya mashambulizi, Atletico waliweza kusawazisha goli kupitia kwa Yannick Carrasco. Kwanini hapa Simeone anastahili kupongezwa tena?

Carrasco aliingia kuchukua nafasi ya Augusto Fernandez wakati wa kipindi cha pili. Carrasco alifanya kazi kubwa ya kuwanyanyasa Real na kufanya mabeki wa timu hiyo kutopanda hasa beki wa kulia.  Alifunga bao hilo zikiwa zimesalia dakika 10 tu kutokana na krosi maridhawa iliyochongwa na beki wa kulia Juanfran na kuifanya game hiyo kwenda muda wa ziada wa dakika 30.

Carrasco alikuwa ni mchezaji aliyejitoa na licha ya kuingia kipindi cha pili lakini ndiye mchezaji aliypiga chenga nyingi kuliko yeyote kwenye mchezo wa jana.

Penati zilizopigwa baada ya dakika 120 kumalizika ndiyo zilipigilia msumari wa uchungu kwa Diego Simeone. Huu ulikuwa ni wakati ambao ama hakika Simeone alitarajia makubwa kutoka kwa vijana wake kutokana na yaliyokea mwaka 2014. Lakini bahati ndiyo ilikuwa haipo tena upande wao na kushindwa kwa mikwaju ya penati.

Kipigo cha jana kilikuwa ni kama shubiri kwa wafuasi wote wa Atletico kuanzia mashabiki, kocha na wachezaji kutokana na kutofikia malengo na matumaini.

Baada ya mchezo huo Diego Simeone aliongea maneno yenye kutia uchungu sana, alisema hivi”Sisi tunajiona ni watu ambao tunaiwakilisha jamii yetu, watu wetu ambao tunapambana kwa ajili yao na hakika tunaendelea kufanya hivyo”. “Tukiacha kufanya hivyo, basi hatutakuwa na nafasi huko mbeleni.” Na kwa sababu nipo na nitaendelea kuwepo hapa Vicente Calderon, Atletico haitoacha kupambana kwa ajili ya kutimiza ndoto za kuchukua taji la Champions League siku za usoni”.