Salim Mbonde-Beki Mtibwa Sugar
Na Baraka Mbolembole
MLINZI wa kati na nahodha msaidizi wa Mtibwa Sugar, Salim Mbonde amemaliza mkataba wake, na baada ya misimu mitatu akiwa na timu hiyo ya Turiani, Morogoro kijana huyo mwenye miaka 21 amesema kuwa hatojiunga na timu yoyote kubwa nchini wakati huu wa usajili na badala yake anatazama kwenda Misri, Ethiopia, Zambia au Afrika Kusini ambako pia anatakiwa na vilabu vya huko.
Katika mahojiano niliyofanya na beki huyo-namba 5 siku ya Alhamis hii, Bonde ameweka wazi kuwa atajifunga tena kwa mwaka mmoja zaidi na Mtibwa kama tu dili za kwenda ng’ambo zitakwama lakini si kujiunga na ‘wababe’ hao wa kandanda nchini ambao wanamuwania tangu mwaka 2014.
Akiwa amecheza game 32 na kufunga magoli mawili na ku-assist mara 6 katika michuano yote (Mechi 26-Magoli mawili, assists 5 katika VPL, Mechi 5 bila goli na assist moja katika Mapinduzi Cup, Mechi moja isiyo na goli wala assist katika FA Cup,) Mbonde alitakiwa kwenda nchini Misri mwezi Disemba katika majaribio na klabu ya Zamalek lakini dili hili lilikwama kutokana na muda, amefunguka mengi kuhusu mwenendo wa ligi kuu msimu wa 2015/16 jinsi ulivyokuwa.
Ungana nami hapa kwa mengi zaidi kutoka kwa kijana huyu zao la Moro Kids-Timu ya vijana Morogoro.
www.shaffihdauda.co.tz: Msimu umekwisha. Unaweza nisaidia takwimu zako, mechi ulizocheza, magoli uliyofunga na hata asissts ulizofanikiwa kutoa pia…
Salim Mbonde; P Ligi kuu-mechi 26 -magoli 2-assists 5 fMapinduzi cup-mechi 5-Magoli 0-assists 1, FA Cup Mechi 1-magoli 0-assists 0. Kwa hiyo kwa ujumla msimu huu nimecheza mechi 32 nimefunga magoli 2 na nimetoa assists 6.
www.shaffihdauda.co.tz: Asante sana, unazungumziaje kuhusu msimu kiujumla. Kama mchezaji-kiongozi ni madhaifu gani umeyaona katika ligi na yaboreshwe vipi ili kuwa ligi bora zaidi ijayo?
Salim Mbonde:
Ligi ilikuwa na ushindani mkubwa msimu huu japo mapungufu hayakosekanagi katika kitu chochote kile mimi nadhani TFF inatakiwa ijirekebishe katika masuala haya yafuatayo;
Upande wa waamuz;
Kwa kiasi kikubwa hawa wameharibu msimu huu ukiangalia mambo mengi yanajirudia lakini maamuzi yanatofautiana kati yao wenyewe. Kwa mfano kadi nyekundu aliyopewa Kessy (Hassan) katika mechi dhidi ya Toto ndiyo kosa hilohilo alilofanya Oscar Joshua mechi ya Coastal na Yanga Tanga, na ndiyohilo hilo alilofanya Yondani (Kelvin) mechi ya Yanga na Ndanda, Taifa , lakini Kessy alipewa kadi nyekundu hao wengine kadi za njano nashindwa kuelewa.
Lakini pia ubovu wa maamuzi yao hayaishi hapo ila pia angalia goli alilofunga Tambwe (Amis) dhidi ya Coastal mshika-kibendera kaona kama kaunawa mpira ila refa amelazimisha liwe goli. Acha hilo angalia goli walilosawazisha Ndanda dhidi ya Mtibwa (Mtwara) duniani kote hamna suala kama lile lakini Nkongo aliweka goli maana Said Mohame ‘Nduda’ alidaka mpira Atupele (Gree) akampokonya mpira ukiwa mkononi mwake na kufunga na goli likakubaliwa mbali na hayo yapo mengi siwezi kuyamaliza ila moja la kusikitisha ni katika Mechi yetu na Kagera, Shinyanga refa mwenyewe ananiambia “ Mbonde nyie hamshuki waachieni wenzenu washind” nilishangaa sana kwa hiyo yapo mengi mengi yakurekebisha kwa upande wa waamuzi.
Ni upangaji mbovu wa ratiba ambao unapelekea watu kuona kama kuna upangaji matokeo vile, ukiangalia msimu huu ligi imepelekwa sana mbele kupisha maandalizi ya timu ya taifa vilabu vilivyokuwa vinacheza mashindano ya Kimataifa, ila mbona inakuwa tofauti kwa wenzetu ambao wameendelea na hao ndio wenye kushiriki mashindano mengi kuliko sisi na ratiba huwa haibadiliki na sijawahi kusikia kwamba tunapisha maandalizi ya mashindano fulani kwa baadhi ya timu ila kwetu kipo.
www.shaffihdauda.co.tz: Kitu gani kimekuvutia katika msimu uliomalizika?
Salim Mbonde: Kitu kilichonivutia ni ushindani wa ligi ulikuwa mzuri nategemea kama utaendelea ligi itakuwa na upinzani zaidi ya hapa.
www.shaffihdauda.co.tz: Safu ya timu gani ya mashambulizi ilikupa wakati mgumu sana, kwanini?
Salim Mbonde: Msimu huu mimi sikupata taabu saana na washambuliaji wa timu yoyote ile, ila nimeona walinzi wengi wakipata tabu wanapocheza na Yanga. Nahisi safu ya Yanga ndiyo ilikuwa bora msimu huu ukiangalia idadi ya magoli waliyofunga washambuliaji wake kwa mfano idadi ya magoli aliyofunga Tambwe (21) Ngoma ( 17) Msuva ( 9) ni idadi kubwa ukilinganisha na safu nyinginezo kama ya Azam FC ambayo una mkuta beki kama Kapombe ana Magoli mengi kuliko washambuliaji.
www.shaffihdauda.co.tz: Mtibwa mlianza msimu kwa ushindi wa game nne mfululizo, nini kimewaangusha kufikia nafasi ya 5 mliyomaliza mwisho wa msimu?
Salim Mbonde: Kwa upande wangu nahisi majeruhi yalituandama sana, ukiangalia Mtibwa haina mbadala wa wachezaji wengi hivyo akiumia mtu muhimu katika kikosi ni shida kubwa.
www.shaffihdauda.co.tz: Umemaliza mkataba Mtibwa, je, ni kweli utajiunga na Azam FC au Simba ambazo zinakuhitaji?
Salim Mbonde: Msimu ujao nataka nicheze nje ya Tanzania ndiyo malengo yangu hayo hivyo sijafikiria kucheza Tanzania ila ikitokea ni kabaki basi nitaongeza mkataba tena Mtibwa wa mwaka tena kuliko kucheza Timu kubwa kwani najua zitanizuia nikitaka kuondoka nje na mimi sina muda mwingi nataka niondoke.
www.shaffihdauda.co.tz: Ni Misri au Afrika Kusini?
Salim Mbonde: Sehemu nazozisikilizia ni nyingi kama vile Ethiopia, Misri, South Africa na Zambia, hivyo itakayokaa vizuri ndio nitakayoenda.
www.shaffihdauda.co.tz: Ni timu inayocheza mabingwa wa Afrika? Au ni Zesco ambako tayari rafikiyako Liuzio yuko huko?
Salim Mbonde: Juma ndiyo ananitafutia nafasi kwahiyo kasema kama itashindikana Zesco basi atanitafutia kwingineko.
www.shaffihdauda.co.tz: Tuombe iwezekane, ikitokea dili za nje zote zikakwama, utabaki Mtibwa?
Salim Mbonde: Nitabaki Mtibwa kwasababu naishi nao vizuri na wananilipa vizuri na pia nipo huru kwenda mahala popote.