SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumapili, 29 Mei 2016

T media news

Mahakama Yataifisha Ng’ombe 1,312 Kwa Kosa la kuchunga ndani ya Hifadhi ya Wanyamapori

MAHAKAMA ya mkoa wa Katavi imetaifisha ng’ombe 1,312 walioingizwa na kuchunga ndani ya hifadhi ya wanyamapori ya Rukwa huku washtakiwa watatu wakinusurika kutumikia vifungo vya miaka miwili jela baada ya kulipa faini kati ya Sh 500,000 na 700,000.

Katika shauri la kwanza mfugaji, Shigera Mayunga (22) amenusurika kifungo cha miaka miwili jela baada ya kulipa faini ya Sh 700,000 katika Mahakama ya mkoa wa Katavi huku ikimwachia kwa masharti mdogo wake, mwenye umri wa miaka 12 .

Washtakiwa hao wawili walitiwa hatiani na mahakama hiyo kwa makosa ya kuingiza ng’ombe 532 na kuchungia ndani ya hifadhi ya wanyamapori ya Rukwa. 

Hakimu Odira Amworo akitoa hukumu hiyo pia aliamuru kutaifishwa kwa ngo’mbe wote 532 na kusema kuwa amelazimika kutoa adhabu kali ili iwe fundisho kwa wafugaji wengine wenye tabia kama hiyo.

Awali Mwendesha Mashtaka, wakili wa serikali Achiles Mulisa alisema washtakiwa hao wawili walitenda makosa hayo Machi , 2016 ambapo kwa pamoja waliingiza mifugo yao na kuchunga ndani ya hifadhi ya wanyamapori ya Rukwa kinyume cha sheria .

Katika shauri la pili wafugaji wawili, Ngusa Keleja “Mtungi” na Charles Mtokambali (40) wamenusurika kutumikia kifungo cha miaka miwili jela baada ya kila mmoja wao kulipa faini ya Sh 500,000 kwa kuingiza ng’ombe 780 na kuchunga ndani ya hifadhi ya wanyamapori ya Rukwa .

Akitoa hukumu hiyo , Hakimu Amworo pia aliamuru kutaifishwa kwa ng’ombe wote 780 na kuwa amelazimika kutoa adhabu kali ili iwe fundisho kwa wafugaji wengine wenye tabia kama hiyo.

Awali Mwendesha Mashtaka, Wakili wa Serikali , Mulisa alisema washtakiwa hao wawili walitenda makosa hayo Machi 25, 2016 ambapo kwa pamoja waliingiza mifugo yao na kuchunga ndani ya hifadhi ya wanyamapori ya Rukwa kinyume cha Sheria.