Waislamu huko Bosnia Herzegovina wamebainisha kusikitishwa na kifungo cha miaka 40 tu jela alichohukumiwa Radovan Karadzic aliyekuwa kiongozi wa zamani wa Bosnia Serbia ambaye amepatikana na hatia ya kuua Waislamu 7,000.
Mahakama ya Kimataifa ya Yugoslavia ya Zamani ICTY yenye makao yake The Hague ilimpata Karadzic na hatia ya mauaji ya kimbari ya Srebrenica mnamo Julai mwaka 1995 ambapo zaidi ya wanaume Waislamu 7,000 waliuawa katika hujuma ya askari wa Bosnia Serbia.
Mahakama hiyo imesema Karadzik akiwa rais wa nchi hiyo alikuwa na uwezo wa kuzuia mauaji ya Waislamu lakini hakufanya hivyo bali alishirikiana na kamanda wa kijeshi Ratko Mladic katika kuwaua Waislamu kwa lengo la kuwaangamiza kwa umati wanaume wote Waislamu huko Srebrenica.
Karadzic alipatikana na hatia ya makosa kadhaa ya jinai dhidi ya binadamu na jinai za kivita.
Hata hivyo manusura na jamaa zaidi ya 150 wa waliouawa wamesema hawakurudhishwa na kifungo hicho. Kada Hotic, naibu mwenyekiti wa jumuiya ya waathirika amebainisha kutoridhishwa na hukumu hiyo na kuongeza kuwa Waislamu wa Bosnia wanahisi uadilifu haukutendeka.
Hatidza Mehmedovic ambaye alipoteza familia yake yote huko Srebrenica amekasirishwa na hukumu hiyo ambayo ameitaja kuwa hafifu. Mehmedovic ambaye hana dada, ndugu wala mume amesema Karadzik ataishi maisha ya kistarehe gerezani huku idiolojia yake ikiendelea kuwepo.