Kusikiliza / Hamishia
Ulezi ndio zao la asili kwa mwezi huu wa Novemba kwa mujibu wa shirika la chakula na kilimo duniani, FAO likisema kuwa nafaka hiyo ni muhimu siyo tu kwa mlo bali pia kwa kuinua kipato cha wakulima wadogo.
Katika tovuti yake FAO imesema unga wa ulezi ambao hujulikana pia kama wimbi, unaweza kutumika kutengeneza mkate, chapati maji, uji, ugali au hata kinywaji na zao hilo lina virutubusho vya madini kama yale ya chuma na Calcium.
Halikadhalika zao hilo halina protini haina ya gluteni na hivyo kulifanya bora zaidi kwa watu wenye uvia na nafaka aina ya ngano zenye protini hiyo.
Kwa wakulima, ulezi pamoja na kwamba kiwango chake cha mavuno kwenye eneo dogo ni kikubwa, pia unaweza kuhifadhiwa kwa miaka miwili bila kemikali zozote hatarishi na ni mwokozi wakati msimu wa mavuno unapodorora.
FAO inasema ulezi ulianza kulimwa katika kaya miaka 5,000 iliyopita huko Ethiopia na Uganda na hatimaye maeneo ya nyanda za chini barani Afrika.
Miaka 3,000 baadaye India ilianza kulima zao hilo na sasa ni kitovu cha matumizi mbali mbali ya nafaka hiyo.