SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumapili, 27 Machi 2016

T media news

Bomba la gesi laneemesha vijiji 126

Katika kuhakikisha kuwa jamii inanufaika na miradi yake, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), linalipa kati ya Sh. 300,000 hadi Sh. 500,000 kwa mwezi kwa kila kijiji kinachopitiwa na bomba la gesi kati ya Madimba, Mtwara mpaka Kinyerezi Dar es Salaam.

Akizungumza mbele ya kamati ya Bunge ya Nishati na Madini iliyoambatana na Naibu Waziri, Medard Kalemani; iliyotembelea miradi ya kuzalisha gesi asilia ya Mnazibay na Madimba, Mtwara:

Kaimu meneja mkuu wa kampuni tanzu inayoshughulika na usambazaji wa gesi nchini, Kapuulya Musomba, alisema fedha hizo zinalipwa kwa vijiji 126 ambavyo vimepewa jukumu la kulinda bomba hilo.

Alisema, hilo ni moja kati ya mengi yanayotekelezwa na shirika hilo kwa jamii inayoishi katika maeneo yanayozunguka miradi ya gesi.

Alisema fedha hizo zinatolewa na serikali kwa sasa kwasababu bado shirika halijaanza kunufaika na fedha zinazotokana na uwekezaji wa miradi hiyo.
“Kwa ajili ya kutengeneza mahusiano ndio hivyo kati ya sh. 300,000 hadi 500,000 kwa mwezi tunaigawa," alisema Musomba. "Kila kijiji kinapewa kutokana na urefu wa bomba ulivyo."

Aidha, alisema changamoto ambayo ilijitokeza katika ulipaji ni kwamba baadhi ya vijiji vilikuwa havina akaunti za benki na vingine akaunti zao zikiwa hazifanyi kazi kiasi cha kusababisha kuchelewa kupata fedha hizo.

Akizungumzia vijiji vya Msimbati na Mnazibay ambako kuna visima vya gesi asilia, alisema zaidi ya asilimia 70 ya wafanyakazi walioajiriwa na kampuni ya uchimbaji wa visima hivyo ya Morel and Prom (M&P), wanatoka katika vijiji hivyo.

“Wakati wa kuchimba hapa nimekaa zaidi ya miezi mitatu hapa, ‘over seventy percent’ (zaidi ya asilimia 70) ya wafanyakazi wanatoka hapo," alisema.
"Shida tu ni kwamba kukiwa na project (mradi) inaajiri watu wengi, kama imeisha wanakuwa wachache.”

Kamati ya bunge ilitembelea Mnazibay ambako kuna mitambo inayozalisha umeme wa gesi asilia unaotumika mkoani Mtwara kuona namna shughuli za uzalishaji zinavyofanyika.

Kabla ya hapo kamati hiyo ilifika katika kisima cha gesi cha Mb3 na baadaye kutembelea kiwanda cha kuchakata gesi hiyo cha Madimba.