Habari sanaa na michezo

Jumapili, 8 Machi 2026

T media news

Jenerali wa kijeshi wa Iran, Mohammad Reza Naqi, ameibua mjadala mkubwa baada ya kutoa kauli kali za kejeli


 Jenerali wa Iran Amkejeli Trump na Mwenzake Netanyahu Baada ya Shambulio Kupiga Kambi Tupu ya Basijh

Jenerali wa kijeshi wa Iran, Mohammad Reza Naqi, ameibua mjadala mkubwa baada ya kutoa kauli kali za kejeli dhidi ya Rais wa Marekani Donald Trump na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kufuatia taarifa za shambulio la kijeshi lililolenga kambi ya wanamgambo wa Basijh nchini Iran.


Kwa mujibu wa Jenerali Naqi, shambulio hilo liliripotiwa kufanywa na ndege ya kivita iliyotoka kwenye manowari ya kijeshi ya Marekani yenye thamani ya mabilioni ya dola. Hata hivyo, alidai kuwa kambi hiyo ya Basij tayari ilikuwa tupu wakati shambulio hilo lilipofanyika.


Akizungumza kwa dhihaka, Jenerali huyo alisema operesheni hiyo inaonyesha kile alichokiita “kushindwa kwa kijeshi na matumizi mabaya ya rasilimali nyingi kwa matokeo sifuri.” Kwa maoni yake, kutumia vifaa vya kijeshi vya gharama kubwa kushambulia eneo ambalo halikuwa na wanajeshi wala vifaa muhimu ni ishara ya mipango mibovu ya kijeshi.


Katika kauli iliyozua mijadala mikali kwenye vyombo vya habari na mitandao ya kijamii, Naqi aliwadhihaki viongozi hao wawili akisema kuwa “akili ya Trump na Netanyahu ni ndogo kuliko akili ya ndege.”


Kauli hiyo ilitafsiriwa na wachambuzi kama jaribio la Iran kuonyesha kuwa mashambulizi ya wapinzani wake hayakuwa na athari kubwa kama ilivyodaiwa.


Matamshi hayo yamekuja wakati mvutano kati ya Iran na washirika wake kwa upande mmoja, na Marekani pamoja na Israel kwa upande mwingine, ukiendelea kuongezeka kufuatia mfululizo wa mashambulizi na vitisho vya kijeshi katika eneo la Mashariki ya Kati.


Baadhi ya wachambuzi wa siasa za kimataifa wanasema kauli za Jenerali Naqi zinaweza kuwa sehemu ya vita vya propaganda kati ya pande husika, ambapo kila upande hujaribu kuonyesha kuwa umefanikiwa au kwamba adui yake ameshindwa.


Wengine wanaona kuwa kauli hizo zinaweza kuongeza mvutano zaidi, hasa katika kipindi ambacho eneo hilo tayari linakabiliwa na hali tete ya kiusalama.


Hadi sasa, hakuna taarifa rasmi kutoka serikali ya Marekani au Israel iliyojibu moja kwa moja madai ya Jenerali huyo wa Iran. Hata hivyo, tukio hilo limeendelea kuzua mjadala mkubwa mtandaoni na kwenye majukwaa ya kisiasa kuhusu ufanisi wa mashambulizi ya kijeshi yanayoripotiwa kufanywa dhidi ya malengo ndani ya Iran.