Bunge la Ethiopia limemchagua Abiye Ahmed kuwa waziri mkuu wa taifa hilo la pili barani Afrika kuwa na idadi kubwa ya watu kufuatia kuteuliwa kwake na chama tawala wiki iliyopita.
Abiye ameapishwa rasmi leo kuwa Waziri mkuu akimrithi Hailemariam Desalegn ambaye alijiuzulu wadhifa huo kati kati ya mwezi Februari baada ya misururu ya maandamano dhidi ya serikali yaliyosababisha vifo vya mamia ya raia wengi wao kutoka maeneo ya Oromia na Amhara.
Abiye mwenye umri wa miaka 42, ndiye mwanasiasa wa kwanza kutoka jamii ya Oromo kuwa Waziri mkuu na kuna matumaini kuwa atatuliza maandamano dhidi ya serikali yaliyozuka tangu mwaka 2015.
Ameahidi kuleta mageuzi, kuanzisha mazungumzo na Eritrea kudokeza kuwa utawala wake utavipa vyama vya kisiasa uhuru zaidi na kuwataka waethiopia walio nje ya nchi kushiriki kikamilifu katika siasa na maendeleo ya nchi.
Waoromo takriban milioni 100, ambao ndiyo wengi zaidi Ethiopia wamekuwa wakilalamika kuwa wanatengwa kisiasa na kiuchumi na utawala.