Utunzaji wa gari unahitaji mambo mbalimbali ambayo ni ya kitaalamu yatakayomsaidia dereva kuwa salama awapo safarini.
Changamoto zinazojitokeza katika utunzaji wa magari zimesababisha kuwapo kwa sehemu maalumu ambazo wamiliki wa magari hupeleka vyombo vyao kwa ajili ya kufanya ukarabati wa aina mbalimbali.
Sehemu hizo zinafahamika kama karakana za kukarabati magari (Gereji).
Gereji ni sehemu au eneo maalumu ambalo limesajiliwa kisheria kwa ajili ya kutoa huduma ya ukarabati wa magari na vyombo vingine vya usafiri ikiwemo pikipiki.
Eneo hili huwa ni maalumu kwa ajili ya kufanya ukarabati wa mambo mbalimbali yanayovikumwa vyombo hivi. Vifuatavyo ni vitu muhimu ambavyo vinatakiwa kuwepo ili kuanzisha Gereji na kuifanya iweze kutoa huduma iliyokusudiwa.
Eneo
Ili uweze kuanzisha gereji, kitu cha kwanza kuzingatia ni kuwa na eneo. Eneo ni kitu muhimu katika uendeshaji wa biashara yoyote.
Hakikisha eneo lako linakuwa rafiki kufikika na wamiliki na madereva wa magari, ili kuweza kuwarahisishia kufuata huduma za ukarabati katika eneo la gereji yako.
Eneo kwa ajili ya gereji ni lazima liwe pana ili kuweza kumudu kupokea magari yote yanayokuja kupatiwa huduma ya ukarabati wa hitilafu tofauti.
Vifaa
Gereji inaweza kutoa huduma nzuri kwa wateja kutokana na uwepo wa vifaa mbalimbali vinavyohitajika katika shughuli nzima ya ukarabati wa magari.
Upatikanaji wa vifaa ni kitu cha muhimu kwa sababu unasaidia kukabiliana na changamoto yoyote ambayo imetokea kwenye gari lililofikishwa katika gereji yako. Hapa tunazungumzia vifaa kama vile spana za ukubwa mbalimbali n.k.
Watu wenye ujuzi na fani ya ukarabati wa magari (mafundi)
Baada ya kupata eneo na vifaa, kitu muhimu ni kuwa na rasilimali watu. Watu hawa wanatakiwa kuwa na ujuzi kwenye fani ya ukarabati wa magari ili waweze kutoa huduma stahiki kwa wateja wanaokuja kwenye gereji yako.
Kwa sasa gereji nyingi hazina wataalamu wa kutosha, kutokana na changamoto ya upatikanaji wa ajira, hivyo mtu akishafahamu kushika spana na kufungua tairi anajiona anaweza kufanya kazi gereji.
Lakini kiuhalisia gereji inahitaji watu wenye ujuzi wa masuala ya magari, kwa sababu hitilafu nyingine katika magari zinahitaji huduma za kitaalamu sana, hivyo usipokuwa na ujuzi wa kutosha unaweza ukashindwa kutatua tatizo katika gari na kusababisha kuongezeka kwa tatizo.
Vifaa vya huduma ya kwnza (first aid kits)
huduma ya kwanza inamaanisha huduma ya msaada inayotolewa kwa mtu anayekabiliwa na ugonjwa au madhara ya ghafla wakati daktari hayupo karibu na kabla hajapelekwa hospitalini kwa matibabu zaidi. Katika gereji vifaa vya huduma ya kwanza ni kitu muhimu kwa usalama wa wafanyakazi wa eneo hilo.
Gereji ni sehemu ambayo inatumia vifaa mbalimbali ambavyo vinaweza kusababisha majeraha kwa mtumiaji. Hivyo ni muhimu kuwa na vifaa vta kutolea huduma ya kwanza kwa mafundi ili linapotokea tatizo iwe rahisi kutoa husuma hiyo.