Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA) imekanusha taarifa zinazosambazwa katika mitandao ya kijamii juu ya uwepo wa nauli mpya zilizopangwa na mamlaka hiyo kwa safari za mabasi yaendayo mikoani.
Taarifa hizo zilizosambazwa mitandaoni zimedai kuwa, uwepo wa nauli hizo mpya za mabasi ya mikoani zimekuja kufuati kupanda kwa gharama za mafuta (dizeli na petroli).
Taarifa iliyotolewa na SUMATRA jana Aprili 14 kwenda kwa abiria, watoa huduma na umma kwa ujumla, imeeleza kuwa, hakuna nauli mpya zilizotangazwa na SUMATRA kwa sasa.
Aidha, wadau wanakumbushwa kuwa, viwango vya nauli kwenda maeneo mbalimbali ya nchi vinaweza kupatikana katika tovuti ya mamlaka hiyo yawww.sumatra.go.tz
Aidha, viwango hivyo vya nauli vinaweza kupatikana kupitia ujumbe mfupi wa maandishi kwa kuandika neno Nauli (acha nafasi), sehemu unapoanzia safari (acha nafasi), sehemu unapokwenda. Kwa mfano, Nauli Dar Tanga, kisha tuma ujumbe huo kwenda namba 15200.