Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mstaafu, Ludovick Utouh, amekosoa hatua ya serikali kutoa majibu juu ya taarifa za ukaguzi wa hesabu zinazotolewa na Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu (NAOT).
Amesema hoja za ukaguzi hazitolewi na mkaguliwa bali mwenye mamlaka ya kufanya hivyo ni CAG mwenyewe baada ya kuridhishwa na utekelezaji wa mapendekezo yake.
Mapema wiki hii, serikali ilianza kujibu hoja za ukaguzi za CAG kutokana na taarifa ya ukaguzi wa taasisi za umma, huku ikisisitiza kuwa inafanya hivyo kwa kuwa imepewa jukumu hilo kikatiba.
Utoah ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Wajibu ambayo inalenga kuhamasisha uwajibikaji na utawala bora nchini, alisema hayo jana katika semina ya siku moja ya kuwajengea uwezo wabunge wa kamati tatu za bunge, mjini hapa.
Kamati hizo ni za Hesabu za Serikali (PAC), Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) na ile ya Uwekezaji Mitaji ya Umma (PIC).Alisema inaonekana sasa hivi hakuna uelewa mzuri kwa Watanzania kuhusu Ofisi ya CAG na majukumu yake.
“Ofisi ile ipo kikatiba. CAG ana jukumu la kukagua mapato na matumizi yote ya serikali na ni jukumu lake kuuambia umma wa Watanzania aliyoyaona, hivyo niseme tu kwamba kuna utaratibu wa yeye kutengeneza hoja za ukaguzi na kutoa hoja za ukaguzi,”alisema.
Alisema inaweza kutokea CAG akaridhishwa na utekelezaji wa mapendekezo yake baada ya uhakiki ndipo hoja ya ukaguzi inafutwa kwenye daftari la hoja za ukaguzi.
Aidha, alisema kuwa anatambua kamati hizo msingi wa kazi yake ni usimamizi na uwajibikaji. Kutokana na jukumu hilo, kuna umuhimu wa kuelewa fika katika ripoti zenyewe kitu gani kinazungumzwa na kuna umuhimu wa kufanya hivyo.
“Madhumuni ya mafunzo haya ni taasisi hii kujitambulisha rasmi kwa kamati za bunge zinazoshughulika na usimamizi na uwajibikaji wa serikali ambapo ndio jukumu kubwa la taasisi yenyewe hii,”alisema Utoah.
Alisema katika semina hiyo watazungumzia pia mambo ya uwajibikaji yaliyojikita kwenye ripoti ya CAG.
Naye Mwenyekiti wa PIC, Raphael Chegeni, alisema taasisi hiyo ina watu waliobobea kwenye masuala ya usimamizi wa fedha na itawawezesha kujua namna ya kusimamia serikali.
“Pia kutambua sisi tuna mchango gani wa kuhakikisha rasilimali za taifa zinatumika vizuri. serikali ya awamu ya tano imejikita kuhakikisha kunakuwa na matumizi mazuri ya rasilimali fedha,” alisema.
Alisema serikali imewekeza zaidi ya Sh. trilioni 48 hivyo ni lazima ipate mrejesho kwenye uwekezaji wake.
Naye, Mwenyekiti wa PAC, Naghenjwa Kaboyoka, alisema mafunzo hayo yatawasaidia kuwajengea uwezo na kutambua wajibu wao.
Alisema kamati ndiyo kiungo kati ya Bunge na serikali kwa ajili ya kuona fedha za umma zinatumikaje na maofisa masuhuli wanahojiwa vipi.
“Hizi hoja za CAG zikishaletwa bungeni zinakabidhiwa, PAC ndiyo inakaa na kuchambua na kuwaita maofisa masuhuli kutoa majibu ya hoja za CAG kwa kamati kutokana na fedha walizopewa.
“Sasa kazi ya CAG anaenda kufanya uhakiki mara baada ya kuwasilishwa majibu ya hoja husika ili kama hoja inafungwa ndiyo inafungwa au kama haifungwi tunaendelea,”alisisitiza.