SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumanne, 13 Machi 2018

T media news

Sababu za mashahidi Kutofika Mahakamani kesi ya Mfanyakazi wa TRA anaemiliki magari 19

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam, imesema itaanza kusikiliza ushahidi wa Jamhuri dhidi ya kesi inayomkabili Ofisa Msaidizi wa Forodha wa Mamlaka ya Mapato Tanzania(TRA), Jennifer Mushi anayekabiliwa na tuhuma za kumiliki magari 19 na kuishi maisha ya juu kuliko kipato chake kama mtumishi yenye thamani ya zaidi ya Sh. milioni 530.8.

Kesi hiyo ilipangwa kusikilizwa jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shahidi.

Hata hivyo, upande wa Jamhuri uliomba mahakama kupanga tarehe nyingine kwa kuwa mashahidi hawajapatikana kutokana na kuwa na majukumu mengine.

Wakili wa Serikali Vitalis Peter alidai kuwa kutokana na mashahidi kuwa na majukumu mengine ya serikali wameshindwa kuwapata kwenda kutoa ushahidi dhidi ya mshtakiwa huyo.

Hakimu alisema mahakama yake itaanza kusikiliza ushahidi wa Jamhuri Aprili 9.

Katika kesi ya msingi, Peter alidai kati ya Machi 21, 2016 na Juni 30 mwaka huo mahali tofauti jijini Dar es Salaam, akiwa mtumishi wa TRA, mshtakiwa huyo alikutwa akimiliki mali zisizolingana na kipato chake, kinyume na sheria ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Alitaja mali hizo kuwa ni magari 19 ya Toyota Rav4, Toyota Dyna Truck, Toyota Vitz, Suzuki Carry, Toyota Ipsum, Toyota Wish, Toyota Mark II, Toyota Regius, Toyota Estima, Toyota Alex, Toyota Noah, Toyota Crown, Toyota Hiace, Toyota Estima, Toyota Passo na Suzuki Carry, yote yakiwa na thamani ya Sh. milioni 197.6.

Katika shtaka la pili, ilidaiwa kati ya Machi 21, 2012 na Machi 30, 2016 jijini Dar es Salaam akiwa mwajiri wa TRA aliishi maisha ya hali ya juu tofauti na kipato chake, yenye thamani ya Sh. 333,255,556.24.

Mshtakiwa alikana mashtaka hayo na yuko nje kwa dhamana.