Upande wa mashtaka katika kesi ya mauaji inayomkabili mke wa bilionea Erasto Msuya, Miriam Mrita (41), umeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kuwa jalada la kesi hiyo bado lipo mikononi kwa mkurugenzi wa mashtaka (DPP) kwa ajili ya kulifanyia uamuzi.
Wakili wa Serikali, Mutalemwa Kishenyi amedai leo Machi 6, 2018 mbele ya hakimu mkazi mkuu, Thomas Simba wakati shauri hilo lilipokuja kwa ajili ya kutajwa.
Mbali na Mrita, mshtakiwa mwingine katika kesi hiyo ya mauaji namba 5 ya mwaka 2017 ni mfanyabiashara Revocatus Muyela (40) na wote wanakabiliwa na shtaka moja la mauaji ya dada yake Erasto Msuya, Aneth Msuya.
Itakumbukwa kuwa, Februari 21, 2018 upande wa mashtaka ulidai mahakamani hapo kuwa jalada la kesi hiyo lipo kwa DPP kwa ajili ya kufanyiwa kazi.
"Shauri lilikuja kwa ajili ya kutajwa na jalada la kesi hii lipo kwa DPP kwa ajili ya kulifanyia maamuzi, hivyo tunaomba tarehe nyingine kwa ajili ya (kesi) kutajwa," amedai Kishenyi.
Baada ya Kishenyi kueleza hayo, wakili wa utetezi, Peter Kibatala amekubaliana na upande wa mashtaka na kuiomba mahakama hiyo kupanga tarehe katika muda mfupi.
Kutokana na maelezo ya pande zote, Hakimu Simba ameahirisha kesi hiyo hadi Machi 13, 2018 itakapotajwa.
Washtakiwa kwa pamoja wanakabiliwa na shtaka la mauaji ambapo wanadaiwa kumuua dada wa bilionea Msuya, Aneth Msuya.
Februari 23, 2017 waliachiwa huru na mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Godfrey Mwambapa na kisha wakakamatwa tena na baadaye kusomewa shtaka moja la mauaji.
Washtakiwa wanadaiwa kumuua kwa makusudi Aneth tukio linalodaiwa kutokea Mei 25, 2016 maeneo ya Kibada Kigamboni jijini Dar es Salaam.