Rais wa Jamhuri ya Afrika Kusini, Jacob Zuma ametangaza kujiuzulu nafasi yake, baada ya kushinikizwa na chama chake cha African National Congress (ANC).
Kamati Kuu ya ANC ilikutana Jumanne na kumtaka Rais Zuma ajiuzulu kabla ya kuisha kwa siku ya Jumatano, kutokana na tuhuma mbalimbali za rushwa zilizokuwa zikimkabili.
Mapema leo mchana Rais Zuma alifanya mahojiano na kituo cha runinga cha Afrika Kusini na kusema kwamba hawezi kujiuzulu kwa sababu wale wote wanaomtaka ajiuzulu hawajaweza kumwambia ni kosa gani amefanya.
Kama Rais Zuma asingejiuzulu, Bunge la nchi hiyo leo Alhamisi lingepiga kura ya kutokuwa na imani na Rais, ambapo kama matakwa ya sheria yangetimia, basi Rais Zuma angeng’olewa madarakani.
Akilihutubia taifa, Rais Zuma amesema kwamba hataki kuona chama tawala, ANC kinagawanyika ikiwa chanzo ni yeye, hivyo ameamua kujiuzulu nafasi hiyo aliyoitumikia tangu mwaka 2009.
Rais Zuma aliingia madarakani baada ya mtangulizi wake Thabo Mbeki kujiuzulu kufuatia kushinikizwa na chama chake.
Kufuatia kujiuzulu kwa Zuma, kiongozi wa ANC, Cyril Ramaphosa anatarajiwa kuapishwa kuchukua nafasi ya kuliongoza taifa hilo.
Licha ya kuchukua uamuzi wa kujiuzulu, Rais Zuma amesema kwamba hakubaliana na namna ANC walivyoshubghulikia suala lake, kwani kwa miaka yote aliyokuwa madarakani amewatumikia raia wa Afrika Kusini kwa uwezo wake wote.