Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga, Hamidu Njovu kumchukulia hatua Mkuu wa Shule ya Sekondari Muhama kwa madai ya kuwachangisha michango ya TZS 5,000 wanafunzi ikiwa ni gharama ya kuwapatiwa fomu za maelezo ya kujiunga na shule hiyo.
RC Wangambo amesema mkuu huyo wa shule iliyopo ndani ya Manispaa ya Sumbawanga mkoani Rukwa achukuliwe hatua kutokana na kitendo chake cha kwenda kinyuma na maagizo yaliyotolewa na Rais Dkt Magufuli, akitaka wanafunzi kutotozwa michango ya aina yoyote.
Agizo hilo limetolewa Februari 2, 2018 wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara katika Kata ya Malangali baada ya baadhi ya wananchi kufichua jambo hilo, na kuonyesha risisti walizokuwa wakipewa baada ya kulipa kiasi hicho cha fedha.
“Tulilazimika kutoa fedha hizi na kupewa stakabadhi kwa kuwa tuliambiwa mwanachi ambaye hatotoa fedha hawezi kupewa fomu hizo na hivyo kukosa sifa ya kujiunga katika shule hii,” amesema mmoja wa wakazi wa eneo hilo.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga, Hamidu Njovu alikana kufahamu kuhusu michango hiyo, mara baada ya kuulizwa uhalali wake.
RC amewaonya walimu kutojihusisha na michango ya aina yoyote kutoka kwa wanafunzi na kwamba kazi yao ni kufundisha.