SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Jumapili, 4 Februari 2018

T media news

AG mpya aahidi makubwa sekta ya sheria

Na Fatma Salum-MAELEZO

Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dkt. Adelardus Kilangi ameahidi kufanya kazi kwa bidii ili kupunguza changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya Sheria hapa nchini.

Akizungumza baada ya kuapishwa katika hafla iliyofanyika jana  ikulu jijini Dar es Salaam, Dkt. Kilangi alisema kuwa changamoto hizo haziishii katika ngazi ya kitaifa tu bali hata kwenye nchi nyingine za Afrika na Jumuiya za Kimataifa.

“Natambua kuwa yapo mambo mengi yanahitaji kufanyiwa kazi na kila nchi katika Afrika ikiwemo Sheria za udhibiti wa rasilimali zetu na mfumo wa Sheria za Kimataifa unaohusu masuala ya uwekezaji,” alisisitiza Kilangi.

Kilangi aliongeza kuwa atahakikisha ofisi yake inazishughulikia kwa karibu changamoto hizo kwa kushirikiana vyema na wadau wengine wa sheria ili kuongeza ufanisi katika Serikali kwa maslahi ya taifa.

“Tunakuahidi Mhe. Rais kwamba tutafanya kazi kwa akili zetu zote, nguvu zetu zote na uwezo wetu wote kwa maslahi ya Watanzania,” alisema Kilangi.

Kwa upande wake Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahim Juma aliwapongeza majaji wapya walioapishwa katika hafla hiyo na kuwaeleza kuwa nafasi ya Majaji wa Mahakama Kuu ni muhimu sana katika taifa hivyo ni wajibu wao kufanya kazi na kufuata sheria bila upendeleo.

Naye Waziri wa Katiba na Sheria Prof. Palamagamba Kabudi alibainisha kuwa mabadiliko aliyofanya Mhe. Rais ya kuwateua Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Naibu wake ni mwanzo tu wa mabadiliko makubwa ambayo amedhamiria kuyafanya katika Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka Mkuu wa Serikali.

Alieleza kuwa lengo la mabadiliko hayo yanayotekelezwa na Rais John Magufuli ni kuongeza uwajibikaji na ufanisi katika utendaji kazi.

“Namuomba Mhe. Rais taratibu zifanyike ili wanasheria wote walioko katika wizara zote za Serikali Kuu warudi chini ya usimamizi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kuimarisha uwezo wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na kuongeza ufanisi,” alisema Kabudi.

Akitoa nasaha zake kwa wateule walioapishwa kwenye hafla hiyo, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Tulia Ackson aliwaasa kutofanya kazi kwa mazowea kwa kuwa yapo mambo mengi yanahitaji maboresho ikizingatiwa kwamba ulimwengu unabadilika kwa kasi kubwa.

Aidha, aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali George Masaju ambaye uteuzi wake ulitenguliwa katikati ya wiki hii ameapishwa kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania na kuahidi kufanya kazi kwa bidii na ushirikiano katika kuwatumikia wananchi na taifa kwa ujumla.

Katika hafla hiyo iliyohusisha kiapo cha utii na kiapo cha maadili walioapishwa ni pamoja na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Dkt. Adelardus Kilangi , Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali Paul Ngwembe na Majaji wawili wa Mahakama Kuu ambao ni George Masaju na Gerson Mdemu.

Kabla ya uteuzi, Dkt. Adelardus Kilangi alikuwa Mkurugenzi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (SAUT) kituo cha Arusha na Paul Ngwembe alikuwa Mkurugenzi wa masuala ya Sheria katika Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA).