WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameweka jiwe la msingi kwenye mradi wa njia ya kusafirisha umeme wa kilovoti 220 kutoka Makambako hadi Songea na kuahidi kuwa Serikali itaendelelea kuwasambazia umeme wananchi wote.
Ametoa ahadi hiyo jana Jumapili, Januari 7, 2018 wakati Akizungumza na wananchi wa eneo la Unangwa nje kidogo ya mji wa Songea, mara bada ya kuweka jiwe la msingi kwenye mradi wa ujenzi wa kituo cha kupozea umeme.
Waziri Mkuu alisema ujenzi huo unaenda sambamba na ahadi ya Mheshimiwa Rais, Dk. John Joseph Magufuli ya kuwataka Watanzania wapate umeme kwa urahisi.
“Mheshimiwa Rais ameshusha gharama za umeme kutoka sh. 380,000 hadi sh. 27,000. Zamani ulikuwa unalipia fomu za kuomba umeme, sasa hivi nazo amesema zitolewe bure. Nguzo za umeme zilikuwa zinatozwa sh. 150,000, sasa hivi amesema zitolewe bure,” alisema.
Waziri Mkuu amesema zamani mikoa ya Njombe, Iringa, Ruvuma, Songwe, Mtwara na Lindi ilikuwa na matatizo sufu ya kupata umeme lakini hivi sasa mikoa ya Mbeya na Iringa imepata suluhisho baada ya kukamilika kwa mradi wa umeme wa kilovoti 400 wa kutoka Iringa hadi Shinyanga.
“Sasa hivi tunaingia Njombe na Ruvuma na baadaye tutaenda Mtwara na Lindi,” alisema.
Alitumia fursa hiyo kuwaomba wakazi wanaoishi jirani na mahali kituo hicho kinapojengwa, wawe walinzi wakuu wa mali za mkandarasi ili mradi huo uweze kukamilika mapema. “Eneo hili lina saruji, nyanya na nondo, si vema watu wachache wjiokeze na kuiba vifaa vya ujenzi. Saidieni kulinda eneo hili, na mali za mkandarasi ili mradi ukamilike kwa wakati,” alisisitiza.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa mradi huo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dk. Titus Mwinuka alisema mradi huo utakapokamilika utaunganisha vijiji 120 na wateja 22,700.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa ofisi za TANESCO mjini Songea ambalo litagharimu sh. bilioni 2.27. Ujenzi wa jengo hilo unatarajiwa kukamilika mwishoni mwa Machi, 2018.
Akimkaribisha kuzungumza na watumishi wa TANESCO na wananchi waliohudhuria hafla hiyo, Waziri wa Madini, Dk. Medard Kalemani alisema jengo hilo ni moja ya majengo makubwa saba nchini ambayo yatakuwa makao makuu ya kimkoa ya TANESCO.
Majengo mengine yatajengwa kwenye mikoa ya Singida, Kilimanjaro, Mtwara, Njombe, Pwani, Geita na Kigoma. “Kukamilika kwa ofisi hizi haimaanishi wafanyakazi wakae ofisini na kufaidi viyoyozi. Ni lazima waende nje kuwafuata wateja,” alisisitiza.
Dk. Kalemani alisema chini ya mradi wa kusafirisha umeme wa kilovoti 220 kutoka Makambako hadi Songea, Serikali imeamua kujenga vituo vya kupozea umeme huko Makambako, Madaba na Songea ambavyo vitakamilika Agosti 30, 2018.
“Kukamilika kwa mradi huo kutaiepusha TANESCO na mzigo mkubwa wa kutumia fedha nyingi kununua mafuta mazito ambao pia utapunguza gharama za umeme kwa watumiaji. Kabla ya hapa, TANESCO ilikuwa inatumia sh. milioni 900 kwa siku kugharimia mafuta hayo,” alisema.
Mapema, akitoa taarifa ya ujenzi wa jengo hilo, Kaimu MKurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Dk. Titus Mwinuka alisema ujenzi wa jengo hilo ambao umefikia asilimia 78, unatarajiwa kukamilika ifikapo Machi 31, mwaka huu.
“Gharama za ujenzi kwa jengo zima ni sh. bilioni 2.198 na gharama za mshauri ni sh. milioni 78 na gharama zote zinafikia sh. bilioni 2.276. Fedha hizi zimetolewa na Serikali,” alisema.