Jumla ya wanafunzi 400 wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu Dar es salaam (DUCE) wamekubali kujitolea kufundisha shule mbalimbali za Manispaa ya Temeke.
Akiongea leo na Kurasa mara baada ya kumalizika kwa semina ya maadili na miiko ya taaluma ya ualimu, mwanzilishi na mratibu wa zoezi hilo Mwl. Amijidius Cornel amesema wanakabiliwa na changamoto ya nauli.
''Tuna changamoto zinazotukabili katika utekelezaji wa majukumu yetu haya ya kufundisha kwa kujitolea hivyo tunaomba serikali itufadhili nauli ili tuweze kuzifikia shule nyingi zaidi'', amesema Mwl. Cornel.
Baada ya kupata semina kuhusu maadili ya ualimu leo, wamesema wamekamilika na wapo tayari kuitumikia elimu ambayo wameipata ili kujijenga na kupata uzoefu utakaowasaidia kuwa bora zaidi hata pindi watakapopata ajira rasmi.
Muhula wa masomo kwa mwaka 2018 unatarajiwa kuanza rasmi Jumatatu ijayo, Januari 8 ambapo walimu hao wataanza kazi katika shule mbalimbali za Manispaa ya Temeke.