SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Alhamisi, 4 Januari 2018

T media news

Ni kweli kwamba huwezi kuwa tajiri bila njia za mkato Tanzania?

TANESCO, sekta ya nishati ni moja ya maeneo yanayoongoza kwa “upigaji” serikalini

Baada ya kuwasilisha maoni yangu juma lililopita, nilithibisha kuwa, si mimi pekee niliye na wasiwasi kuhusu hali ya baadhi ya wafanyabiashara nchini. Nilipata maoni mengi kutoka kwa watu wenye uelewa wa mambo, ambao nao walionyesha kuchukizwa na watu ambao wameiibia nchi yetu, wameiba fedha za wananchi walipakodi ambazo zingewasaidia kwa mambo mbalimbali.

Nilishtushwa na kushangwa na maoni ya baadhi ya watu waliokuwa wanasema kwamba, huwezi kuwa tajiri bila kuiba. Sikubaliani na kundi la watu wenye mtazamo huu, kwani kwa Tanzania, ni lazima, na tunaweza kufanya mambo kwa usahihi.

Kama ukipata utajiri wako kwa njia zilizo halali, utapongezwa, lakini ukiupata katika njia za kiujanja ujanja, lazima utachunguzwa. Hivyo ndivyo ilivyo.

Kama haujafanya lolote baya, na unaweza kuthibitisha hilo, sheria ipo upande wako na haujapoteza kitu chochote. Hadi hapo tumehitimisha mjadala huo, sasa tusonge mbele.

Rais na serikali anayoiongoza ameonyesha ushirikiano wake na kuisaida sana TAKUKURU na taasisi nyiingine za serikali ili zifanye kazi kwa niaba yetu, na kuhakikisha kila mwananchi anafanya mambo yake kwa mujibu wa sheria.

Baada ya kuweka hilo akilini, ningependa sasa kuongeza masuala machache katika barua yangu ya juma lililopita, iliyokuwa na kichwa cha Habari, “Kuelekea 2018, Barua yangu kwa Rais wangu Magufuli”. Unaweza bado kuisoma hapa.

Tangu alipoingia madarakani zaidi ya miaka miwili iliyopita, Rais Dkt Magufuli amefanya kuwa mkakati wake mpango wa kutokomeza rushwa, na tunapaswa kushukuru kwa hilo.

Siku yake ya kwanza ya urais, alifanya ziara ya kushtukiza katika Wizara ya Fedha na Mipango. Lakini pia, alifuta maadhimisho ya sherehe za uhuru na kuwataka watu kufanya usafi ili kutokomeza ugonjwa wa kipindupindu. Tumeona mambo makubwa na yakupongezwa aliyofanya katika Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari, Mamlaka ya Mapato Tanzania na namna alivyoongeza uhuru na kuipa meno TAKUKURU.

Kila juma tunapata taarifa mpya kuhusu watu wanaochunguzwa na TAKUKURU kuhusu tuhuma za rushwa. Kwa miezi michache iliyopita, tumeona waalimu, madaktari, wanasiasa na hata mawaziri wa zamani wakichunguzwa.

TAKUKURU ya sasa yenye nguvu, chini ya uongozi wa Valentino Mlowola imefanikiwa kuokoa fedha za umma kiasi cha TZS 60.3 bilioni katika miaka miwili ya fedha iliyopita. Kama mwaka mmoja una siku 365, basi miaka miwili ina siku 730. Ukichukua shilingi bilioni 60.3 ukagawa kwa siku 730, unapata kwamba kila siku katika miaka miwili iliyopita TAKUKURU wamekuwa wanaokoa shilingi milioni 83 sawa na shilingi milioni 3.4 kila saa. Pesa ambayo ingeliwa na wajanja katika rushwa serikalini.

Ilani ya Chama cha Mapinduzi mwaka 2015 imeeleza kuhusu kuleta maendeleo kwa wananchi, hivyo kuokolewa kwa kiwango hicho cha fedha ni hatua moja kubwa ya kutimiza ahadi hiyo.

Mapema mwezi Aprili 2017 nilisoma Makala moja ambapo Kamishna Mlowola alisema kwamba, ni imani yake, kwa kupambana na rushwa kikamilifu kutasaidia kupandisha hali ya maisha ya wananchi, na umasikini utaanza kupungua taratibu.

Huu ni mwaka muhimu sana kwa Rais wetu. Ni mwaka ambao anafikia nusu ya muhula wake atakaokaa madarakani, ni mwaka ambao watu wataanza kutazama na kutoa maoni yao kuhusu namna anavyofanya kazi.

Tumeona kwa macho yetu kwamba serikali imejipanga kupiga vita rushwa, lakini sasa tunataka kuona tutafaidika na nini kutokana na vita hii. Hizo shilingi milioni 83 kwa siku zinazookolewa zina tafsiri ipi katika maisha yetu.

Kama nilivyosema katika chapisho langu la mwisho, kuna watu ambao wamefanikiwa kukwepa adhabu. Katika mwaka 2018 ambao ndio tumeuanza, hatuwezi kuwaacha watu hawa hasa wanaoendelea kuficha fedha zao ughaibuni au kwa njia nyingine, kuendelea kuiba rasilimali za nchi yetu. Tanzania inastahili kilicho bora.

 

Mpaka wakati mwingine,

 

Wanzagi Tiliro