Edward Lowassa amekwenda Ikulu in his individual capacity (kama mtu binafsi). Lowassa alikuwa mgombea urais wa Tanzania kupitia muungano wa UKAWA mwaka 2015, hiyo haina maana kuwa yale ayafanyayo kati ya 2016 - 2020 yanawakilisha mawazo, matakwa, utashi na mapenzi ya wananchi na wafuasi wa vyama vilivyomo kwenye UKAWA. Na haina maana kuwa yanawakilisha mawazo ya watanzania.
Jambo la kukumbushana ni kuwa, Edward anazo haki zote "as a Tanzanian and an individual" (kama mtanzania na mtu binafsi) kuomba appointment na RAIS na kuzungumza chochote watakacho at individual level (ngazi za watu binafsi) au at individual vs institution capacity (ngazi ya mtu binafsi vs taasisi/rais/ikulu).
Mjadala wetu unapaswa kuwa ajenda. Je, Lowassa amekwenda Ikulu kwa ajenda ipi? Je, Rais alikuwa na ajenda ipi at the same time? Bwana Yule alikwenda ikulu immediately baada ya uchaguzi wa Magufuli, alikwenda kumpongeza Magufuli na kumpa sifa nyingi, Bwana Yule alikwenda at his individual capacity just like what Lowassa did (kama mtu binafsi kama alivyofanya Lowassa) - tofauti yao inaweza kuwa AJENDA, Bwana Yule alikuwa na ajenda ipi na ENL alikuwa na ipi.
Hadi sasa tunafahamu kuwa kilichooneshwa kwenye vyombo vya habari, taarifa ya ikulu na hata video zinazosambazwa zinaonesha Lowassa akisisitiza kuwa alikwenda Ikulu kumpongeza Rais kwa kazi nzuri anayofanya. Ni jukumu la wasaidizi wa Lowassa au Lowassa mwenyewe aidha kutoa taarifa ya ufafanuzi na kuueleza umma yale aliyozungumza na Rais na hayasemwi kwenye taarifa ya ikulu, au kukaa kimya ili yale yaliyoripotiwa na ikulu ndiyo yawe AJENDA iliyompeleka ikulu.
Kama haya yanayoripotiwa na yanayooneshwa kwenye hizi video ndiyo yaliyompeleka Lowassa ikulu basi yeye Lowassa kama mtu binafsi amefanya hivyo kwa utashi na uhuru wake na tuuheshimu. Kwa kawaida ikulu ni mahali pazito na penye mtu mkubwa na majukumu mengi, na unapokwenda lazima uwe na ajenda zito na yenye maana kwa taifa zima.
Rais ni mtu mkubwa, ni mtu ambaye ukichukua dakika zake tano uwe umezungumza naye kuhusu usalama wa nchi, uchumi, ajira, demokrasia, ujenzi wa taasisi, mgawanyo wa madaraka, haki za binadamu, utawaka bora, mapambano dhidi ya umasikini, maradhi na ujinga.
Mimi binafsi nimekwenda Ikulu zaidi ya mara 10 wakati wa Kikwete. Mara zote hizo kwa vikao vya wazi na vya ndani tulikuwa tuna ajenda ya katiba mkononi. Kusingekuwa na ajenda ya katiba au ajenda nyingine nzito, mimi nisingelifika ikulu. Rais Kikwete yako mambo mengi mazuri alifanya, mengine mengi aliboronga, just like what Magufuli does!
Kwenda ikulu ni jambo zuri na la heri lakini kuna msingi ukiwa una ajenda. Ikulu watu hawaendi kumpongeza Rais, huenda kumpa mawazo mapya na kumkumbusha pale asipofanya sawasawa, just like what we did with president Kikwete.
1. KUPONGEZANA kwa Lowassa na Magufuli hakutaondoa ukweli kuwa Tundulissu yuko kitandani na watanzania wanataka kujua wauaji wa Lissu ni kina nani na walitumwa na nani mchana kweupe?
2. KUPONGEZANA kwa Lowassa na Magufuli hakutaondoa ukweli kuwa Rais Magufuli amepiga marufuku shughuli za vyama vya siasa huku chama chake kikiendelea na shughuli hizo waziwazi chini yake.
3. KUPONGEZANA kwa Lowassa na Magufuli hakutaondoa ukweli kuwa nchi yetu kwa sasa inanyimwa uhuru wa kutoa maoni na kuikosoa serikali katika masuala ya msingi, bunge limewekwa mfukoni, vyombo vya habari viko kitanzini na raia wanasakwa na kufungwa kwa sababu wametoa maoni yao.
4. KUPONGEZANA kwa Lowassa na Magufuli hakutaondoa ukweli kuwa uchumi wa nchi umeyumba sana na umasikini umekithiri. Takwimu za serikali zinaonesha uchumi unakua kwa kasi ya JET lakini mtaani hali ni mbaya sana, biashara zinakufa, mabenki yanafungwa, ajira hakuna, mitaji hakuna na mzunguko wa pesa umefariki dunia.
5. KUPONGEZANA kwa Lowassa na Magufuli hakutaondoa ukweli kuwa hali ya usalama wa nchi ni mbovu mno, miili ya watu inaokotwa ikielea baharini na mitoni, wapo watanzania wametekwa na hawajulikani walipo na watu wanaoikosoa serikali wamekuwa wakiwindwa, kutishwa na kufuatiliwa.
6. KUPONGEZANA kwa Lowassa na Magufuli hakutaondoa ukweli kuwa nchi inahitaji KATIBA MPYA, katiba ambayo itajenga mustakabali salama wa ujenzi wa taasisi imara ambazo hazitayumbishwa na mtu au mamlaka yoyote kwenye utendaji wake.
7. KUPONGEZANA kwa Lowassa na Magufuli hakutaondoa ukweli kuwa vita dhidi ya rushwa na ufisadi inasuasua sana, mla rushwa/mtoa rushwa "A" anakamatwa, "B" anaachwa huru, "C" anatishwa na kulindwa "D" anapandishwa cheo n.k. kumekuwa na double standard ya kutosha huku dola ikitaka watu wote waimbe kuwa inapambana na rushwa.
8. KUPONGEZANA kwa Lowassa na Magufuli hakutaondoa ukweli kuwa wao wawili siyo the ABSOLUTE TRUTH of Tanzanians (ukweli mkuu na halisi wa watanzania), watanzania wana ukweli wao, ukweli wa maisha yao na ukweli wa ndoto zao za baadaye, Lowassa na Magufuli hawakuwahi na hawatakuwa na hati miliki ya FUTURE na NDOTO za watanzania.
9. KUPONGEZANA kwa Lowassa na Magufuli hakutaondoa ukweli kuwa mfumo wa uendeshaji wa uchaguzi ndani ya nchi yetu ni wa kibabe, mbovu, usio na tija na usiokubalika katika kusimamia uchaguzi huru na haki na kwamba mfumo huo usiporekebishwa utatuletea matatizo makubwa ya kidemokrasia.
10. KUPONGEZANA kwa Lowassa na Magufuli hakutaondoa ukweli kuwa watanzania wanataka ajira, mazingira ya kujiajiri, mitaji, masoko, maliasili ziwanufaushazo, uhuru wa maoni, haki za msingi za kiraia, utawala bora, demokrasia, bima za afya, fedha mifukoni n.k.
Haijalishi Lowassa na Magufuli wamepongezana kiasi gani, jambo la msingi ni walikuwa na ajenda ipi kubwa ya kujenga usimamizi wa ajenda za watanzania.
Mimi nawaheshimu wote wawili, walikuwa wagombea urais waliotikisa sana miaka miwili iliyopita - lakini wote wawili tunao uhuru wa kuwasema tutakavyo, kuwakosoa tutakavyo na kuwahoji tutakavyo.
Wale vijana wenzangu ambao nimeona wanapambana kutuaminisha kuwa Lowassa amezungumza kwa niaba ya watanzania alipokutana na JPM, na kuwa amewa-shame UKAWA na wana mabadiliko, tafuteni ajenda nyingine mpya.
Lowassa amekwenda IKULU on his own, on his agenda, heshimuni ajenda yake, heshimuni uamuzi wake, yeye ni mtanzania tu. Hojini uzito wa ajenda yake na tuishie hapo.
Juzi Babu Seya alikuwa Ikulu, kushukuru kwa kupata msamaha, Babu Seya si msemaji wa wafungwa ambao hawakupata msamaha na si msemaji wa wale watakaofungwa kesho na kesho kutwa.
Muacheni Lowassa atumie uhuru wake, lakini msisahau kuwa Watanzania wanazo ajenda za kudumu, na wataendelea kuzipigania Lowassa akiwepo au asipokuwepo, na wataendelea kuzipigania Magufuli akiwepo au asipokuwepo.
By Mtatiro J
(Haya ni maoni yangu binafsi, hayawakilishi maoni ya chama changu wala nafasi yangu ndani ya chama.)