Unapoendesha gari barabarani, unatakiwa kuzingatia sheria na kanuni zinazowaongoza madereva ili kuepuka adhabu mbalimbali ikiwemo faini na kufungiwa kuendesha vyombo vya moto.
Mambo ya kuzingatia ili kuepuka adhabu ni mengi sana, lakini hapa chini tumeorodhesha vitu 16 ambavyo vitakusaidia kuepukana na adhabu.
1. Hakikisha una leseni yako mkononi, kuwa nayo kwenye gari.
2. Hakikisha umebaba kadi ya gari au ipo kwenye gari lako, nakala halisi au iliyothibitishwa (certified copy).
3. Hakikisha tairi zako ni nzima, bodi la gari yake halijatoboka au kuchanika kiasi cha kuhatarisha usalama wa watumiaji wengine wa barabara.
4. Hakikisha una kizimio moto hai (fire extinguisher) na mikanda kwenye gari yako ni misafi na inafanya kazi.
5. Hakikisha rangi ya kwenye bodi ya gari yako ndio ile iliyoandikwa kwenye kadi ya gari na sio umefanya mabadiliko bila kurekebisha kwenye kadi.
5. Hakikisha gari lina vibali vyote muhimu kutegemeana na aina ya gari na kazi zake.
6. Ikiwaka taa ya NJANO hakikisha unasimama, na sio kukimbilia kupita kabla haijawaka nyekundu.
7. Hakikisha umefunga mzigo wako vizuri ili usiweze kudondoka barabarani au kujeruhi wengine wakati unaovateki. Mzigo usizidi bodi la gari yako.
8. Hakikisha taa zako, hasa za breki zinafanya kazi vizuri, kila inapowezekana tembea na taa ya ziada (spare).
9. Hakikisha unakuwa mvumilivu kwenye foleni, USIJARIBU KUTANUA.
10. Hakikisha hauyapiti (overtake) sehemu ambazo mistari inakataa kuovateki.
11. Heshima alama za barabarani mfano simama kwenye alama ya waenda kwa miguu ili kuwapisha wavuke.
12. Kwa jiji kama la Dar es salaam, hakikisha mara nyingi unatembea 50kph, isipokuwa sehemu ambazo mwendo wa magari unaongozwa na askari. Kwa mikoani jitahidi kuangalia kwa makini alama na kuendesha kwa mujibu wa alama.
13. Usiegeshe sehemu usiyokuwa na uhakika kuwa panaruhusiwa kuegesha.
14. Kama gari lako ni kubwa na la biashara, hakikisha una reflekta za utepe zimebandikwa kuzunguka gari lako (3M).
15. Panga safari zako mapema, na ondoka mapema ili kuepuka kukimbi sana barabarani ukazidisha spidi ukaandikiwa faini.
16. Hakikisha wewe mwenyewe unafunga mkanda kwenye gari, unahimiza abiria wako kufunga mkanda, na pia haujatumia kilevi.