Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limeewahakikishia wananchi kuwa tatizo la kukatika kwa umeme litabaki kuwa historia baada ya kupata ufadhili wa kujenga mitambo ya kuzalisha umeme kutoka serikali ya Japan.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wajumbe wa TANESCO amesema kuwa JICA wameahidi kujenga mtambo ya kufua umeme megawatt 300 ambao utaingizwa katika gridi ya taifa hali ambayo itasaidia kuondoa kabisa tatizo umeme katika mikoa hiyo iliyoko kusini mwa nchi.
“JCIA watajenga mitambo ya kufua umeme wa megawatt 300 hapa Mtwara na kuna shirika jingine la kijapani linaitwa Sumitomu na kwa sasa hivi wanajenga mtambo wa megawatt 240 pale kinyerezi,” amesema Mhandisi Alexander Kyaruzi.
Kwa Upande wa Mkurugenzi wa kiwanda cha kuchakata gesi cha Madimba, Sultan Pwaga ameeleza kuwa uzalishaji wa umeme unategemea sana ongezeko la mahitaji na kuwahakikishia wananchi wa maeneo ya Mkuranga kupata umeme wa uhakika baada ya mitambo ya umeme ya Kinyerezi Two kuanza uzalishaji wa umeme.
“Tunaongeza kulingana na demand kwa hiyo tunategemea Kinyerezi Two ambayo mitambo yake imeanza kufanya kazi. Ikianza uzalishaji basi na sisi huku tutaongeza uzalishaji na wateja wetu wengine ambao wataongezeka, kwa mfano Dangote na wateja wengine ambao wapo eneo la Mkuranga,” amesema Sultan Pwaga.
Katika kipindi cha takribani miezi mitatu iliyopitaa, maeneo mbalimbali ya nchi yamekabiliwa na tatizo la kukatika katika kwa umeme ambalo limechangiwa na upungufu wa kiwango cha umeme kinachozalishwa hapa nchini.