SASA UNAWEZA DOWNLOAD T MEDIA NEWS APPS.

Alhamisi, 21 Desemba 2017

T media news

Taharuki Yatanda Baada ya Fuvu la Binadamu Kukutwa Mgodini

WACHIMBAJI wadogo wa dhahabu katika mgodi wa kikundi cha Kapumpa walipatwa mshtuko juzi baada ya
kukuta fuvu linalosadikiwa kuwa la binadamu wakati wakiendelea na shughuli hiyo wilayani Sikonge mkoani Tabora.

Akizungumza na Nipashe jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Wilboad Mutafungwa alisema tukio hilo lilitokea juzi mchana katika kata ya Kitunda.

Mutafungwa alisema Polisi mkoani Tabora inafanya uchunguzi kujua pamoja na mambo mengine, fuvu hilo ni la nani, alifariki katika mazingira gani na lini.

Kamanda Mutafungwa alisema fuvu hilo liligunduliwa na wachimbaji hao wakati wakichimba madini ya dhahabu na kwamba halikuwa na kiwiliwili chake.

Wachimbaji waliokutana na fuvu hilo wakati wakichimba mgodi huo wa dhahabu walitoa taarifa katika kituo kidogo cha Polisi cha Lukula, alisema Kamanda Mutafungwa na kwamba askari kutoka kituo hicho walifika mara moja katika eneo la tukio na kukuta fuvu hilo likiwa ndani ya shimo.

Mutafungwa alisema Polisi imefungua jalada la uchunguzi na kwamba mpaka sasa hakuna mtu yeyote ambaye anashikiliwa ili kusaidia upelelezi wa shauri hilo.

Matukio ya mabaki ya binadamu kukutwa migodini ni nadra japo pamekuwa na minong'ono kuwa baadhi ya wachimbaji mahala pengine hutumia viungo vya binadamu kwa lengo la kuongeza bahati ya madini kimazingara.  Agosti 29, mwaka huu makandarasi wanaofanya ukarabati wa Uwanja wa Taifa, Jijini Dar es Salaam walidai kukuta fuvu la kichwa cha binadamu wakati wakiondoa nyasi za zamani katika eneo la kuchezea mpira uwanjani hapo.

Uwanja huo ulikuwa ukifanyiwa ukarabati kwa kuwekwa nyasi mpya katika sehemu ya kuchezea na haukuwa ukitumiki kwa mechi za ligi kuu ya Bara.

Mei 3, mwaka huu mganga wa kienyeji, Moshi Mohamed Matimbwa (26) na msaidizi wake aliyetambulika kwa jina la Ally Omari Mapande (23) wakazi wa wilayani Kibiti mkoani Pwani walikamatwa na Polisi wa doria baada ya kukutwa na fuvu la binadamu.

Watuhumiwa hao walidaiwa kuwa walikuwa safarini kutoka Mkuranga kwenda Kibiti kwa pikipiki na kwamba waliposimamishwa katika kijiji cha Jaribu walikutwa wakiwa wameficha fuvu hilo kwenye begi.

Aidha, Februari 12, 2015 raia mmoja wa Ubelgiji alikamatwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) akiwa na fuvu la binadamu. Raia huyo, Balcjan Christine Weejktgns (49) alikamatwa saa 2:00 usiku wakati akikamilisha taratibu za kuingia kwenye ndege ya kuelekea Zurich, Uswisi kisha Ubelgiji.

JUU YA DARIMwanzoni mwa miaka ya 2010, fuvu la binadamu lilikutwa likiwa limefichwa juu ya dari katika nyumba ya mtu mmoja wilayani Same mkoani Kilimanjaro.

Aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro wakati huo na sasa Mkurugenzi wa Upelelezi wa jeshi hilo (DCI), Robert Boaz alisema askari waliokuwa wakisaka wauzaji wa gongo na bangi, walipekuwa nyumba ya Saidi Fundi na kukuta fuvu la kichwa cha binadamu, likiwa limefichwa juu ya dari katika nyumba yake.

Alisema baada ya mahojiano baina ya askari na mtuhumiwa huyo, alisema fuvu hilo ni la baba yake mzazi, Hamisi Elidina aliyefariki dunia miaka ya 1970 na kuzikwa katika eneo la Kifaru wilayani Mwanga.

Alisema mtuhumiwa huyo, alifikia uamuzi wa kufukua kaburi la baba yake kutokana na maagizo ya mizimu ya ukoo wao, kuwa akifanya hivyo atakuwa na maisha mazuri.

Tukio la ajabu zaidi linalohusu fuvu la binadamu lilihusisha Jeshi la Polisi mkoa wa Morogoro kuwafukuza kazi askari wake watatu wa kituo cha Dumila wilayani Kilosa kwa tuhuma za kumbambikizia kesi mfanyabiashara Samson Mwita mkazi wa mji huo kuwa alikutwa na fuvu la kichwa cha binadamu Mei 23, 2013.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Morogoro wakati huo Faustine Shilogile alisema hatua ya kuwafukuza askari hao ilifikiwa baada ya uchuguzi kukamilika na askari hao kuonekana kufanya shughuli ya upekuzi kwa mfanyabiashara huyo bila kuwa na kibali kutoka kwa maofisa wao wa kazi.

Aliwataja askari hao kuwa ni mwenye namba D 4807 D/SSGT Sadick wa kituo kidogo cha Polisi Dakawa, E 4344 SGT Mohamed na E 3821 CPL Nuran wote wa kituo kidogo cha polisi Dumila.

Pia alisema uchunguzi wao umebaini kuwa askari hao walifanya kitendo hicho kwa kushirikiana na raia Rashidi Ally mkazi wa Mbagala jijini Dar es Salaam.

Kukutwa na kiungo chochote cha binadamu ni kosa kisheria.